Tuesday, October 9, 2012

RIPOTI YA MWANGOSI N UTAFITI AMA MAAMUZI YA OFISI FULANI

TAARIFA YA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANDISHI WA HABARI WA CHANNEL TEN BW. DAUD MWANGOSI

1.0 UTANGULIZI


Mnamo tarehe 03 Septemba mwaka 2012, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (MB) aliteua Kamati ya watu watano kufanya uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi, kilichotokea tarehe 02 Septemba 2012, katika Kijiji cha Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa. Kituo cha kazi cha marehemu Daud Mwangosi kilikuwa mkoa wa Iringa ambapo pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa (IPC).

Wajumbe wa Kamati hiyo ni:

Jaji (Mst.) Steven Ihema – Mwenyekiti

Bibi Pili Mtambalike – Mjumbe

Kanali (Dkt. Eng) Wema Wilson Wekwe – Mjumbe

Bwana Theophil Makunga – Mjumbe

Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Juma. Mngulu – Katibu

Sekretarieti ya Kamati ni:

Bi. Edith T. Assenga – Wizara ya Mambo ya Ndani

Bwana Nasoro H. Msumi – Wizara ya Mambo ya Ndani

2.0 HADIDU ZA REJEA

Kamati ilipewa Hadidu za rejea zifuatazo:

- Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba, 2012 na kuwepo kwa uvunjifu wa amani.

- Kama yalikuwepo makubaliano au maelekezo kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano nchini katika kipindi cha Sensa.

-Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha kifo cha Marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu hiyo na tukio.

-Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha kuna madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia.

-Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa endapo vyama hivyo havitaridhika na amri hizo.

-Hali ya Mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika Utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.

3.0 MUDA WA UCHUNGUZI

Kamati ilipewa muda wa siku 19 kuanzia tarehe 11 Septemba 2012 iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha Ripoti yake ifikapo tarehe 02 Oktoba 2012.


4.0 NJIA ZILIZOTUMIKA KUFANYA UCHUNGUZI:

4.1 Mahojiano na watu mbalimbali waliokuwepo kwenye tukio.

4.2 Kupitia nyaraka na vielelezo mbalimbali.

4.3 Kutembelea eneo la tukio.

4.4 Majadiliano na vikundi mbalimbali (viongozi wa dini ngazi ya kijiji na wilaya hadi ya mkoa; viongozi wa vyama vya siasa kwenye ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa na Taifa, viongozi wa serikali ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa, Taifa) na wanakijiji wa Nyololo.

5.0 UCHUNGUZI

Kamati ya Uchunguzi ilifanya mahojiano na watu mbalimbali ikiwa pamoja na watendaji wa serikali hususan Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya wilaya Mufindi na mkoa wa Iringa viongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa vyama vya Siasa, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Waandishi wa Habari na wananchi wa kawaida (ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa).

6.0. YALIYOJITOKEZA

Baada ya Kamati kukutana na makundi ya watu mbalimbali katika Mkoa wa Iringa na Viongozi wa Vyama vya Siasa wa kitaifa jijini Dar es Salaam, mambo kadhaa yalijitokeza na baadhi yao ni:

-Hofu ya kutoweka kwa amani miongoni mwa viongozi na wananchi hasa katika mikutano na maandamano ya siasa ambayo yameanza kuota mizizi ya uvunjifu wa amani na mengine kusababisha mauaji. Viongozi na wananchi wengi waliotoa maoni yao mbele ya Kamati wameonyesha hofu kuwa hali hiyo isipodhibitiwa mapema inaweza kulipeleka pabaya Taifa letu.

-Kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na Jeshi la Polisi mkoani Iringa.

-Uwepo wa utashi wa makusudi/dhati kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya vyama.

-Umuhimu wa Ushirikiano na mahusiano baina ya vyombo vya serikali, vyama vya siasa, wanahabari na wananchi kwa ujumla badala kuonyeshana ubabe ambao umetufikisha hapo.

- Haja ya kufanya mabadiliko ya kisheria katika mfumo wa usimamizi na utendaji wa masuala ya siasa nchini

- Haja ya kuwa na mabadiliko ya kimfumo katika Jeshi la Polisi badala ya ulioko sasa ambao kwa maoni ya baadhi ya watu waliozungumza na Kamati ni wa kitaifa zaidi na kuacha serikali za mitaa bila ya wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zao.

-Kwamba nguvu kubwa inatumika na vyombo vya dola/usalama dhidi ya raia na hivyo kupunguza imani ya jamii kwa vyombo hivyo.

-Kupungua kwa maadili/uzalendo miongoni mwa Watanzania kuanzia viongozi hadi wananchi hususan kwenye shughuli za kisiasa.

-Haja ya kusisitiza elimu ya uraia kwa jamii kuanzia kwa watoto hadi kwa watu wazima hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi ili kujenga umoja wa kitaifa.

-Kuwepo kwa mikutano na maandamano ya vyama vya siasa yasiyokuwa na kikomo.

-Muonekano wa Jeshi la Polisi mbele ya jamii.

7.0. MATOKEO YA UCHUNGUZI KUTOKANA NA HADIDU ZA REJEA

7.1 Kuhusu “Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo, Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012 na kuwepo uvunjifu wa amani”, uchunguzi wa Kamati umebaini yafuatayo:

Tarehe 30 Agosti 2012 CHADEMA iliandika barua, Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mufindi kutoa taarifa kuhusu ratiba ya mikutano ishirini na sita (26) kwenye majimbo ya Mufindi Kusini na Kaskazini tarehe 02-03 Septemba 2012. Awali ratiba ya mikutano hiyo ilikubaliwa, lakini baadaye siku hiyo ya tarehe 01 Septemba 2012 mikutano hiyo ilisitishwa kwa barua Kumb. Na MFG/A.24/9/54 kutokana na kuongezwa siku za zoezi la Sensa ya watu na Makazi hadi tarehe 08 Septemba 2012.

CHADEMA walikataa kusitisha ratiba ya mikutano hiyo kama inavyothibitishwa na Justin Leornard Mpotwa Katibu wa Wilaya ya Mufindi kwa barua yake Kumb. Na CDM/M4/002/Vol.01/2012 ya tarehe 01 Septemba 2012 kuwa “pia tunaomba ieleweke bayana kwamba kisheria shughuli zetu hazina mwingiliano na wala kuhusiana na program iliyoongezwa ya Sensa. Kwa barua hii tunakuarifu kuwa mikutano tuliyokutaarifu kuifanya kuanzia kesho tarehe 02 septemba 2012 itaendelea kama ilivyopangwa – CHADEMA VEMA”.

Aidha kuwepo kwa zuio la mikutano ya Siasa ya CHADEMA Mkoani Iringa wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linathibitishwa na Amri ya Utendaji (Operation Order) ya Kamanda wa Polisi Mkoa (SACP Michael Kamuhanda) ya tarehe 01 Septemba 2012. Amri ya Utendaji ambayo ni amri halali ilitolewa ili “kuzuia shughuli za Siasa (mikutano na maandamano) kipindi cha zoezi la kitaifa la Sensa kuanzia tarehe 25 Agosti 2012 hadi 08 Septemba 2012”. Uhalali wa Amri/Zuio hili ulithibitishwa pia na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini katika barua yake Kumb Na. DA. 112/ 123/ 01/ 34 ya tarehe 28/08/2010 na wakati wa mahojiano na Kamati ya uchunguzi tarehe 22 Septemba 2012.

Licha ya zuio/amri hii Viongozi wa CHADEMA walikataa kutii amri hiyo. Kutokana na taarifa hizi, Kamati ya Uchunguzi inathibitisha kwamba hapakuwepo na uhalali wa mkusanyiko/mkutano ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012. Kuhusu kuwepo kwa uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012 Kamati ya Uchunguzi ilibaini mambo yafuatayo:

-Tukio la kuuawa kwa Daud Mwangosi jioni ya tarehe 02 Septemba 2012 lilitokea baada ya Operesheni ya Jeshi la Polisi kumalizika. Hii ni kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Iringa na Joseph Senga Mpiga picha/Mwandishi Tanzania Daima.

- Kitendo cha kutotii amri halali ya Kamanda wa Polisi kuagiza wafuasi wa CHADEMA watawanyike kutoka kwenye eneo la ofisi ya Kata ya CHADEMA ilikuwa chanzo cha vurugu.

Uamuzi wa CHADEMA kung’ang’ana kukusanyika isivyo halali eneo la Nyololo ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Dkt. Slaa, Katibu wa CHADEMA uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Den Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya”. Dr. Slaa. : ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani. CHADEMA ndiyo Chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012.

7.2 Kama yalikuwepo makubaliano kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano nchini katika kipindi cha Sensa. Katika kuzungumzia hoja hii tukianzia na Uongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa, Kamati ya Uchunguzi ilithibitisha kuwepo kwa maagizo ya kusimamisha mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa wakati wa kipindi cha Sensa ya Watu na Makazi yaliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, na kuongezwa muda wa Sensa hadi tarehe 08 Septemba 2012 na Kamishna wa Sensa hapo tarehe 01 Septemba 2012.

Aidha hoja hii imethibitika kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa barua yake yenye Kumb Na DA. 112/ 01/ 34 ya terehe 28 Agosti 2012 kwenda kwa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa akiwasihi kusimamisha shughuli zote za mikutano na maandamano ya Vyama vyao kwa kipindi chote cha Sensa ya Watu na Makazi. Aidha kwa mujibu wa Gazeti la Serikali Na 29 VOL 93 ya tarehe 20 Julai 2012, Mhe. Rais, JAKAYA MRISHO KIKWETE kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu namba 14 cha Sheria ya Takwimu sura 351 alielekeza kwamba Sensa ya Watu na Makazi itafanyika kuanzia tarehe 26 mwezi wa nane, mpaka tarehe 08 mwezi wa tisa mwaka 2012.

Kamishna wa Sensa aliratibu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kumalizika ifikapo tarehe 01 Septemba 2012. Hata hivyo kutokana na tathmini aliyofanya, kazi hiyo ilikuwa imekamilika kwa asilimia 95%. Hivyo tarehe 01 Septemba 2012 alitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kwamba ili kila mwananchi apate nafasi ya kuhesabiwa watu watakaokuwa wamesalia ambao ni chini ya 5% wanaombwa kutoa ushirikiano ili zoezi hili likamilike. Hivyo, wale wote mmoja mmoja waliobakia wataendelea kuandikishwa hadi tarehe 08 Septemba 2012.

Kwa upande wake Inspekta Jenerali wa Polisi kwa ujumbe wa simu Kumb Na S8.7/ 2/ A/ VOL XIV/ 59 ya tarehe 28/08/2012, pia simu yake Kumb Na C.28/ B/ 44 ya terehe 01/ 09/ 2012 aliwaelekeza Makamanda wa Polisi wa Mikoa kutoruhusu mikutano na maandamano wakati huu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi mpaka litakapokamilika tarehe 08 Septemba 2012.

Kimsingi Kamati ya uchunguzi imethibitisha kwamba maelekezo kwa Vyama vya Siasa kutoendesha shughuli za mikutano ya hadhara au maandamano yalitolewa kwa mujibu wa Sheria.

7.3 Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha, kifo cha marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu hiyo na tukio.

Hoja kuwa Polisi walitumia nguvu kubwa katika kudhibiti mkutano wa CHADEMA iliungwa mkono na Viongozi wa Serikali ya Kijiji, Viongozi wa dini na Viongozi wa siasa Kijijini Wilayani na Mkoani pamoja na Waandishi wa Habari. Hata hivyo Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa na Viongozi wa Jeshi la Polisi waliona nguvu hizo ni za mazingira ya hali ilivyokuwa.

Uchunguzi wa suala hili umebaini kwamba tarehe 02 Septemba 2012 muda wa saa 10 za jioni huko eneo la Sokoni, Kijiji cha Nyololo kulikuwepo na mkutano usio halali ulioandaliwa na viongozi wa CHADEMA. Upo ukweli kwamba uongozi wa Polisi ulitoa ilani kuamuru wafuasi wa CHADEMA waliokuwepo mkutanoni hapo waondoke la sivyo nguvu itatumika. Walikaidi amri hiyo na ilipoagizwa viongozi wakamatwe ndipo walianza kurusha mawe kwa Askari Polisi. Baadhi ya Askari walijeruhiwa, akiwamo G 9934 PC Mgaka alivunjwa mkono wa kulia. Pia kofia (helmet) tatu ziliharibiwa.

Kutokana na hali hiyo amri ya kupiga mabomu ya machozi na ya kishindo ilitolewa, kwa mujibu wa Kifungu 77 hadi 79 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 – R.E 2002. Operesheni hii ilimalizika baada ya kukamatwa viongozi na wafuasi wa CHADEMA jumla yao saba.

Baada ya zoezi hilo kukamilika Askari Polisi walioshiriki kwenye Operesheni waliamriwa kuingia katika magari tayari kwa kuondoka. Wakati Askari wakipanda kwenye magari kishindo kikubwa kilitokea umbali wa zaidi ya mita 100 kutoka sehemu ambayo operesheni ilikuwa inafanyika na iligundulika kwamba kishindo kile kimesababisha kifo cha Mwandishi wa Habari Daud Mwangosi.

Upelelezi wa awali pamoja na picha za mnato unaonyesha kwamba marehemu alikuwa amemkumbatia Mkuu wa Polisi Kituo cha Mafinga ASP Assel Mwampamba na huku akiwa amezungukwa na Askari Polisi wasiopungua sita ambao licha ya kumzunguka marehemu Daud Mwangosi kuna madai yaliyotolewa na mwandishi wa Habari Joseph Senga kwamba, Askari Polisi hao walikuwa wanamshambulia marehemu kwa kumpiga, ndipo askari mmoja aliyetambuliwa kuwa ni G 2573 PC Pasificus Cleophace Simon alifyatua Bomu la kishindo na kusababisha kifo cha Daud Mwangosi.

Tukio hili linaweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni wileamapamebas(mni ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud Picha Namba 15: Askari Polisi wakimpiga Marehemu Daud Mwangosi, huku OCS M wenye kifimbo) akijaribu kuwazuia. Mwangosi. Katika tukio la kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni Tukio hili linaweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni lile ya Operesheni ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud Mwangosi.

Katika tukio la kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni tatu ambapo ni askari wasiozidi thelathini. Kwa maelezo yaliyotolewa na Mwandishi wa Habari mbele ya Kamati, Bw Joseph Senga anaeleza kuwa watu walishatawanyika na hali kutulia mara baada ya Operesheni hii kukamilika na Polisi kujiandaa kuondoka kwenye eneo la tukio. Tukio la mauaji ya Daud Mwangosi lilisababishwa na kupigwa bomu la kishindo.

Maswali ya kujiuliza katika tukio la mauaji ni Je, kulikuwepo na uwiano unaolingana na tukio hili?, Je Palikuwa na uhalali wa kutumia Bomu la kishindo?, na Je, utumiaji wa Bomu hilo ulikuwa na umuhimu?

Kulingana na tukio lenyewe majibu ya maswali hayo ni kama ifuatavyo:

-Hapakuwa na uwiano wa Bomu na tukio la mauaji, kwa vile utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali mita 80 mpaka mita 100.

-Hapakuwa na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.

- Hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji tayari Askari Polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.

Kwa misingi hiyo Kamati imeona kwamba nguvu iliyotumika mwanzo hadi kumaliza Operesheni haikuwa kubwa. Kuhusu tukio la kuuawa Bw. Daud Mwangosi na kuumizwa baadhi ya Askari Polisi halikustahili kabisa.

7.4 Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia.

Katika kupata ukweli wa jambo hili, Kamati ilikutana na wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa na pia iliwahoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Nyigesa Ramadhani Wankyo na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia mkoani Iringa Said Abdallah Mnunka.

Pia, wakati Kamati inakutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ilileta suala la mahusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na watendaji wakuu wa serikali wa mkoa wa Iringa.

Katika mkutano na waandishi wa habari, ilionekana kuwa katika thathmini yao uhusiano kati yao na Polisi hapo mkoani ni mbaya sana. Walieleza matukio kadhaa ya kunyanyaswa waandishi wa habari wakati wapo kazini, ikiwamo kupigwa, kutishiwa kuharibiwa na kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na hata kutishiwa maisha ili wasiripoti mambo ambayo Polisi wana maslahi nayo.

Kwa mfano, mwandishi wa habari wa Star TV, Oliver Moto alieleza Kamati kuwa: “Waandishi wa habari hawana mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi, na hata wanapofika ofisi za Polisi huwa hawapewi ushirikiano. Kutokana na uhusiano mbaya wanahabari walifanya maandamano tarehe 06 Machi 2012 kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na Jeshi la Polisi hapa Iringa”.

Mwandishi mwingine wa habari Zulfa Shomari ambaye anaandikia gazeti la Mwananchi alieleza kuwa kuna matukio kadhaa ambayo Polisi wamewazuia waandishi kufanya kazi zao mojawapo ni lile ambalo Polisi walikataza kupigwa picha tukio la kukamatwa kwa pembe za ndovu.

Kamati pia iielezwa na mwandishi wa habari wa ITV, Bw. Laurian Mkumbata mkasa wa kuvunjwa kamera yake na OCD Iringa kwenye tukio moja. Ilibidi OCD alipe kamera hiyo kwa maagizo ya RPC.

Pia walisema kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa hivi sasa ana mawasiliano duni sana na waandishi wa habari na juhudi za wengi wao kumfuata ili athibitishe tukio zimekuwa zikishindwa kwani ameweka maagizo getini kuwa mtu yeyote ambae anataka kumuona ni lazima aeleze anataka kumuona kwa sababu gani ndipo aruhusiwe kuingia. Kwa sababu hii waandishi wa habari wengi wamekata mguu kwenda ofisini kwake.

Mwandishi mmoja wa Ebony FM Bw. Raymond Francis, aliiambia Kamati kuwa yeye binafsi alitishiwa kuuawa na baada ya kuandaa kipindi kuhusiana na watu wanaoshukiwa kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya ambao wanahusiana na baadhi ya Polisi wasio waadilifu.

Mwandishi wa Habari Greyson Mgoi wa gazeti la Kwanza Jamii aliiambia Kamati kuna tukio la kuanguka kwa lori la mafuta eneo la Ifunda karibu na Mafinga ambapo waliwakuta wananchi na polisi wakichota mafuta kutoka kwenye hilo gari.

Alisema kuwa waliamua kupiga picha tukio hilo lakini Polisi waliwakamata na kuwalazimisha wafute hizo picha walizopiga. Kwa kuogopa shari walikubali kuzifuta na wakaruhusiwa kuendelea na safari yao.

Waandishi wa Habari hata hivyo walibainisha kuwa uhusiano wao na Polisi hapo mkoani ulikuwa mzuri sana kipindi cha uongozi wa RPC Advocate Nyombi. Walisema kuwa wakati wa RPC Nyombi, alikuwa na utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari na pia alikuwa anafikiwa na waandishi wa habari kwa urahisi kwa simu au ofisini kwake. Walisema lakini ulianza kuharibika alipohama na nafasi yake kuchukuliwa na RPC Mangara na kuwa mbaya zaidi alipokuja Kamuhanda. Walidai kuwa Polisi wa Iringa si waadilifu na wamekuwa wakijiona kama miungu watu.

Waandishi walieleza Kamati, kitu kilichowaudhi sana ni yale majibu yaliyotolewa na RPC baada ya mauaji ya Daud Mwangosi ambayo yalionekana yalikuwa ni ya kupanga ili ukweli usijulikane. Walisema kama si picha zilizotolewa na waandishi wa habari waliokuwepo kwenye tukio, hawadhani kama umma wa Watanzania wangepata ukweli wa tukio hilo.

Walisema tarehe 06 Machi 2012, walifanya maandamano ili kupinga manyanyaso ya Polisi wa mkoani Iringa yaliyopokelewa na Mkuu wa Mkoa. Waandishi wa Habari mkoani Iringa pia walionyesha masikitiko yao kuwa tangu kutokee kwa mauji ya Daud Mwangosi, hawajapokea pole kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake wa juu hata kama ni ya “kinafiki”.

Kwa upande wa pili, yaani Jeshi la Polisi, Kamati ilipata taswira tofauti. RPC Kamuhanda alisema kuwa yeye anaona mahusiano ya Polisi na waandishi wa habari kwa ujumla ni mzuri na yeye binafsi amekuwa akikutana na waandishi wa habari takriban kila siku asubuhi saa nne kuwapa habari. Pia aliiambia Kamati kuwa waandishi wa habari walishiriki kikamilifu katika kuripoti michuano ya mpira ya Kikombe cha Kamuhanda yaliyofanyika mjini Iringa.

Msimamo huo pia ulichukuliwa na viongozi wa juu wa kiutawala akiwemo Mkuu wa Mkoa Dkt. Christine Ishengoma, Katibu Tawala wa Mkoa Bibi Getrude Mpaka ambao walisema kuwa hapakuwa na uhasama wowote kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Waandishi wa Habari. Wote wawili walisema kuwa walimfahamu marehemu Daud Mwangosi na aliteuliwa katika kamati kadhaa za kimkoa ikiwa ni pamoja na ile ya kuandaa Sensa ya Watu na Makazi Mkoani, Kamati ya Masuala ya Katiba ya Mkoa na Kamati ya Kukuza Utalii ya Mkoa.

Kuhusiana na hisia kuwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake hawakujumuika na waandishi katika msiba wa Daud Mwangosi, Dkt. Ishengoma alisema si kweli hawajatoa rambirambi zao kwa kifo cha Mwangosi lakini alitoa pole kwa waandishi wakati ameenda na IGP Mwema kijijini Nyololo na pia kupitia radio katika kipindi kilichotayarishwa na mwandishi wa habari Francis Godwin.

Baada ya kuongea na pande hizo mbili, Kamati imebaini kwamba kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari polisi mkoani Iringa. Kuhusu madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao jeshi la polisi limepanga kuwashughulikia.

Kwenye tukio la Nyololo ambapo mwandishi wa habari Daud Mwangosi aliuawa, mwandishi wa habari mwengine Godfrey Mushi alipigwa na Polisi na inasemekana kujeruhiwa vibaya na baadaye kukamatwa na Polisi.

Kwa mujibu wa Joseph Senga mpiga picha/mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima ambaye alikuwepo kwenye tukio na kupiga picha, alimuona marehemu akipita nyuma ya gari moja la Polisi ambalo lilikuwa na baadhi ya wanachama wa CHADEMA. Punde tu alimwona mtu amezungurukwa na askari akipigwa lakini hakujua ni nani na yeye aliendelea kupiga picha tukio hilo mpaka nae alipokamatwa na Polisi watatu ambao walimwuliza kama nae anataka aende kuungana na mtu anayepigwa pale.

Senga alisema wakati kipigo kinaendelea, kuna askari mmoja mwenye nyota tatu (OCS Mwampamba) aliteremka kutoka kwenye gari na kwenda pale ambapo Yule mtu aliyekuwa anapigwa huku akiwaambia “mwachieni, mwachieni, namfahamu mimi huyo ni mwandishi wa habari!”

Senga alisema mara alisikia kishindo kikubwa na wale askari ambao walikuwa wanamshikilia walikimbia ndipo yeye akaendelea kupiga picha sasa za marehemu Daud Mwangosi ambaye alikuwa amekwisha sambaratishwa na bomu. Alieleza kuwa alimsikia yule askari ambaye alikuja kumsaidia marehemu Mwangosi akisema “afande wameniuwa”, “afande wameniuwa”, akimwambia RPC ambaye alikuwa karibu nae kwani nae aliumizwa vibaya katika mlipuko huo. Senga aliiambia Kamati wale wote ambao walikuwa wame mzunguka marehemu kama wanavyoonekana kwenye picha alizopiga walikuwepo wakati anapigwa.

Maelezo ya Bw. Senga yanatofautiana sana na yale yaliyotolewa na RPC na OC FFU kuwa Marehemu alimvamia OCS Mwampamba na kuwa wale askari huenda walidhania kuwa mkubwa wao alikuwa amevamiwa ndipo walipoamua kwenda kumsaidia. OCS Mwampamba mwenyewe wakati akihojiwa na Kamati ilipokuwa Mafinga alisema hakumbuki kitu.

Hata hivyo, kwa maelezo ya Bw. Senga, ambayo yanakubaliana na yale ya RPC na OC-FFU, kitendo cha kupigwa na mauaji ya marehemu Daud Mwangosi kilitokea baada ya kuisha ile operesheni ya kusambaratisha mkutano wa CHADEMA na hapakuwa na mabishano yeyote au purukushani iliyotokea kabla ya marehemu kuzungukwa na kuanza kupigwa.

Kwa minajili hii basi Kamati imeshindwa kubaini baada ya kumalizika operesheni na askari Polisi kuanza kuondoka, kwa nini Mwangosi alishambuliwa kwa kipigo kabla ya kulipuliwa na bomu la kishindo?

Kwa nini kuna maelezo yanayokinzana kati ya Bw. Senga ambaye alikuwa karibu sana na tukio na yale ya RPC na OC-FFU ambao katika maelezo yao kwa Kamati walisema kuwa wao walikuwa mbali kidogo na tukio kwa hiyo hawakuweza kuona kwa dhahiri kilichotokea. Maelezeo ambayo yalirudiwa na viongozi wa juu wa Polisi ikiwa ni pamoja na Kamishna wa Upelelezi (DCI) Robert Manumba na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema katika mahojiano na Kamati.

Uchunguzi wa Kamati haukuweza kupata ushahidi wa kubainisha kama kupigwa kwa waandishi hao kulitokana na njama yeyote ya Polisi kuwashughulikia au ilitokea kwenye purukushani ya vurugu zilizotokea baada ya FFU kuamriwa kutawanya wanachama wa CHADEMA.

Pia Kamati haikupata ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa mauaji ya Daud Mwangosi yalikuwa ni ya kupangwa. Kutokana na maelezo ya hapo juu, Kamati inapendekeza yafuatayo:-

-Taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu unaostahiki za upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya vyombo hivyo muhimu katika mkoa;

-Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya hatari/ghasia;

-Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi;

- Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa;

- Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla hajauawa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria;

- Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.

- Viongozi wa polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina ili zisipotoshe jamii.

7.5 Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa ambapo Vyama hivyo havitaridhika na amri hiyo.

Sheria Namba 5 ya 1992 kama ilivyorekebishwa na Sheria Namba 7 ya 2009 inaratibu mahusiano ya kiutendaji kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa. Kwa mujibu wa Sheria hii Jeshi la Polisi limepewa madaraka ya kutoa zuio kwa maandishi na kuweka bayana sababu za kuzuia mikutano au maandamano. Zuio aina hii ni halali kwa mujibu wa Sheria na ni sherti Chama cha Siasa kiheshimu na kutii. Fungu la 11 vifungu vidogo Na 1, 4, 5, 6, 7 na 8 ya Sheria ya Vyama vya Siasa likisomwa pamoja na mafungu Namba 43, 44, 45 na 46 ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary Forces Act Sura 322 vitatumika kusimamia uendeshaji mikutano ya Vyama vya Siasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na kwamba Vyama vya Siasa vinatakiwa kutoa taarifa na siyo kuomba idhini, Jeshi la Polisi limepewa uwezo na madaraka juu ya mikutano hiyo kuhusu kuzuia au kuruhusu na au kutoa maelekezo stahiki, kama vile kupendekeza, na kushauri eneo mbadala na tarehe tofauti ya kufanya mikutano/maandamano.

Aidha kutotii amri/zuio ya Jeshi la Polisi ni kosa la Jinai kwa mujibu wa Fungu la 74 la Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 RE.

Vilevile kwa mujibu wa Fungu la 43 (6) ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary Forces Act, Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye Mamlaka ya Rufaa dhidi ya amri/zuio linatolewa na Jeshi la Polisi.

Pamoja na kuwepo kwa Sheria hizi mbili bado kuna mapungufu katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Siasa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa mfano pamoja na madaraka aliyonayo Msajili wa Vyama vya Siasa ya kukifuta Chama cha Siasa kwenye rejesta ya usajili kwa mujibu wa Fungu la 19 na 20 ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kusimamisha utoaji wa ruzuku na matumizi yake, uratibu wa shughuli za vyama hivyo hauko mikononi mwake.

Wadau wanashauri umuhimu wa kuimarisha uhusiano katika shughuli za utendaji kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi ili kudumisha utulivu na amani na utii wa sheria bila shuruti kwa upande mmoja na kukuza mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa kwa upande mwingine.

7.6 Hali ya mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.

Kamati ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi katika kupata majibu kwa hadidu hii ya rejea, ilizungumza na viongozi wa vyama vya siasa kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa na Viongozi wa kitaifa jijini Dar es Salaam na viongozi wa dini kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa.

Kwa ujumla, kila kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi zote ambaye Kamati imezungumza naye kuhusu hadidu hii ya rejea, ameelezea umuhimu wa Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao na wangependa jeshi hilo liachwe huru katika kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa na wanasiasa ili lifanye kazi zake kwa weledi na uadilifu.

Hata hivyo taswira iliyojitokeza ni kwamba kuna mgawanyiko wa mtizamo kuhusu jinsi Jeshi la Polisi linavyoshughulikia mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanaamini kuwa Jeshi la Polisi linakipendelea Chama cha Mapinduzi na kubinya vyama vya upinzani, huku viongozi wa CCM kutoka ngazi ya kijiji hadi Taifa wakilisifia Jeshi hilo kuwa linafanya kazi yake vizuri na kwa weledi mkubwa.

Mgawanyiko wa taswira kuhusu madai kuwa Jeshi la Polisi kuipendelea CCM hauko tu kati ya vyama vya upinzani na CCM bali pia kwa viongozi wa dini kuanzia ngazi za kijiji, wilaya hadi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa hawajasikia hata siku moja mtu anauawa na Polisi kwenye mkutano wa CCM. Mwandishi mmoja alitoa udadisi wake kuwa huwa wanapata shida sana kuandika habari za mikutano ya CHADEMA kutokana na jinsi Polisi wanavyojipanga kwenye mikutano ya chama hicho.

Kudhihirisha umuhimu wa Jeshi la Polisi katika jamii, hata wale wanaolituhumu kuwa linakipendelea CCM, katika kutoa maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa askari wanaoharibu sifa ya Jeshi hilo, wanapendekeza kuwa askari wahusika wachukuliwe hatua na kuomba Jeshi hilo liendeshwe kwa weledi hasa inapotokea askari akalazimika kutumia silaha kukabiliana na fujo isifikie kuua.

Kwa mfano, Mchungaji Peter Katanga wa Revival Baptist Church, alishauri chombo cha Polisi kisitumike kufanya mauaji, au kisitumike na mtu, watu, au kikundi chochote kufanya matendo yasiyo mazuri kwa jamii kwa sababu chombo hicho kipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wote na mali zao.

Viongozi wa siasa wengine bila kujali itikadi zao, wameonekana kukerwa sana na tabia ya watu kuuawa wakati Jeshi la Polisi linatuliza ghasia na hii ikiachiwa iendelee inaweza kuleta uvunjifu wa amani katika nchi. Kwa mfano, Mchungaji wa Kanisa la EFATA Nyololo, Mkombozi Kiliwa alishauri Polisi watumie njia zinazofaa kukabiliana na wanaovunja sheria na si kuua.

Pia Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyololo, Obby Kimbale, alielezea kutokukubaliana kwake na kitendo cha mauaji ya Daud Mwangosi, alipendekeza elimu ya uraia itolewe kwa jamii nzima vikiwemo vyombo vya dola, viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao ili kila mtu kwa nafasi yake akaelewa namna ya kutimiza wajibu wake ndani ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Kwa upande mwingine, wengi waliotoa maoni yao juu ya mahusiano ya Polisi na vyama vya siasa, pamoja na kulaumu Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa katika kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA, pia waliwalaumu viongozi wa chama hicho, kwa kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi hatimaye kusababisha Polisi kutumia nguvu kiasi hicho.

Kitendo cha kuuawa kwa Mwandishi wa Habari, Daud Mwangosi na tabia ya kutokea mauaji katika mikutano ya CHADEMA kimeonekana kuwakera viongozi wengi wa vyama vya siasa kwani wanaamini kuwa Polisi huwa wanatumia nguvu kubwa kupita kiasi ‘wanapotuliza ghasia’ katika mikutano ya CHADEMA.

Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa, Zakaria Mwansasu alielezea sababu ya matukio ya namna hii kuwa ni kutokana na mmomonyoko aliouita mkubwa wa maadili hasa katika vyama vya siasa na akashauri viongozi wa vyama vya siasa wakapewa elimu ya uraia.

Maoni mengi ya viongozi wa vyama vya siasa yamejikita zaidi katika hofu ya nchi kuingia kwenye vurugu na kutoka kwenye kisiwa cha amani na hivyo kutoa uashauri kwa viongozi wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kuweka mbele maslahi ya taifa.

Mchungaji Yokonia Koko wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alielezea ukosefu wa maadili kwa baadhi ya askari Polisi kuwa umetokana na jeshi hilo kuajiri vijana ambao hawana maadili na kwamba watuhumiwa wa mauaji kwenye matukio yanayolihusisha Jeshi la Polisi wakati wa kuzuia fujo katika mikutano/maandamano ya vyama vya siasa wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa askari wengine.

Kasi ya CHADEMA kuendesha mikutano katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kujiimarisha kichama, imepokewa kwa hisia tofauti na vyama vingine vya siasa. Wakati kuna makundi ya watu katika jamii wakidhani kuwa hiyo ni haki yao kama chama cha siasa kinachotaka kukua na kukubalika kisiasa, wengine wanaiona mikutano hiyo ya hadhara ya CHADEMA kama ni kuwapunguzia muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo hasa baada ya kipindi cha uchaguzi kumalizika.

Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama, alishauri kufanyiwa marekebisho kwenye sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 itakayoweka wazi shughuli za vyama vya siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Alisisitiza kuwa shughuli za siasa baada ya Uchaguzi Mkuu zihamie bungeni kwa wanasiasa kuhoji mipango ya maendeleo ya serikali na matumizi ya rasilimali za nchi na wananchi waachwe wachape kazi zao za maendeleo.

Kuhusu Jeshi la Polisi, Mukama alisema mfumo uliopo wa Jeshi hilo unalifanya lionekane la kitaifa zaidi na kushauri libadilishwe kimuundo ili liweze kutandaa hadi serikali za mitaa kuongeza nguvu katika mpango wa ulinzi shirikishi ulioanzishwa na Jeshi hilo.

Mwanasiasa John Shibuda alizungumzia mahusiano kati ya vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kwa kutoa lawama kwa vyama vya siasa kuwa havitoi malezi kwa wanachama wake ambayo yatawafanya wawe waadilifu, wazalendo, waaminifu na watiifu wa sheria.

Alisema vyama vya siasa havina mfumo wa kujihakiki, kujikosoa na kujiwajibisha na akapendekeza kuanzishwa kwa mfumo huo kisheria ambao utawajibisha vyama vya siasa kwa matendo ya viongozi au wanachama wao.

Shibuda alifafanua kwamba sheria anayopendekeza iwe na nguvu ya kutoa adhabu kwa chama cha siasa na kwa kiongozi au mwanachama ambaye atathibitika kuwa ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani.

Kuhusu Jeshi la Polisi mwanasiasa huyo alipendekeza kufanyike kwa marekebisho ya utendaji ili wakuu wa wilaya na mikoa waondolewe nguvu za kiutawala ambazo huwafanya wakati mwingine kutoa maagizo ya kisiasa kwa Jeshi la Polisi na hatimaye kulifanya Jeshi hilo lionekane linatekeleza maslahi ya wanasiasa badala ya kuwa chombo cha kulinda amani.

Kwa ujumla Kamati kutokana na maelezo mbalimbali ya Viongozi wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi, imeona kuwa kuna mahusiano hafifu kati ya baadhi ya Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi.

Kwa kuwa taasisi zote hizi ni wadau muhimu wa amani na utulivu nchini, Kamati inapendekeza:

-Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo na kupunguza migongano.

-Kuhusu madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe Tume, Kamati imeona kuwa zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza endapo kuna mashaka ya kifo hicho.

-Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya kisheria ili kuziba mianya inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya kisiasa.

-Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.

-Kwa kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa raia na mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa zinaleta msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi

8.0. MAONI NA MAPENDEKEZO:

Kutokana na uchunguzi uliofanyika kupitia mahojiano na Viongozi wa kada mbalimbali, kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa, Kamati ina maoni na mapendekezo yafuatayo:

MAONI:

-Kuhusu madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe tume, Kamati imeona kuwa zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza endapo kuna mashaka ya kifo hicho.

-Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.

-Kwa kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa raia na mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa zinaleta msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi

-Kuhusu operesheni ya uzuiaji wa mkutano wa CHADEMA usio halali Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012, Jeshi la Polisi lilitekeleza wajibu wake ipasavyo na kutumia nguvu sahihi. Operesheni iliyoandaliwa na kufanyika ilikamilika kwa kuwatawanya watu waliofika kwenye mkutano, kukamata baadhi ya Viongozi na wafuasi wa CHADEMA na hali ya utulivu ilirejea kwenye eneo husika.

MAPENDEKEZO

-Mauaji ya mwandishi wa habari Daud Mwangosi yalitokea baada ya operesheni kumalizika, na amri ya kuondoka kwa askari eneo la tukio kutolewa na Viongozi wa operesheni hiyo

-Jamii wakiwemo Viongozi waelimishwe umuhimu wa utii wa sheria, kanuni na taratibu ili kudumisha amani na utulivu hapa nchini. Viongozi wengi walionyesha hofu ya kuliingiza Taifa kwenye machafuko makubwa na uvunjifu wa amani iwapo jamii haitazingatia umuhimu wa kutii sheria, kanuni, taratibu na amri halali za Mamlaka.

-Msajili wa Vyama vya siasa afafanue majukumu ya vikundi vya Ulinzi vya Vyama vya Siasa kama vile Green Guard, Red Brigade, Blue Guard.

-Iwepo programu mahususi ya Elimu ya Uraia nchini ili kujenga uzalendo na kukuza maadili ndani ya jamii wakiwemo viongozi wa kada mbalimbali. Hivi sasa jamii inashuhudia kutoweka kwa uzalendo na kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii.

Njia zifuatazo zitumike:

- Elimu ya uraia iimarishwe katika mitaala ya elimu kuanzia Shule za msingi hadi Vyuo Vikuu.

- Uamuzi wa kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana utekelezwe mapema.

- Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Tasnia ya Habari na Taasisi zisizokuwa za Serikali zishiriki kikamilifu katika uenezi wa Elimu ya Uraia nchini.

- Kuhimiza uzingatiaji wa weledi katika utendaji kazi kwa mujibu wa taaluma na miongozo inayotolewa kuleta ufanisi. Aidha elimu endelevu sehemu za kazi itiliwe mkazo.

-Kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya 1992 ili kuweka wazi shughuli za Vyama vya Siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Lengo ni kuwa Shughuli za Siasa zihamie Bungeni kujadili na kuhoji mipango ya Serikali na matumizi ya rasilimali za nchi. Kwa kufanya hivyo wananchi watapata nafasi kufanya kazi za maendeleo.

-Kuboresha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, hususan uanzishwaji wa ofisi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kuratibu ushirikiano/mahusiano baina ya serikali (Jeshi la Polisi) na Vyama vya Siasa. Lengo ni kukuza mahusiano na kuondoa mgongano.

-Utaratibu wa kufanya mikutano mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari uimarishwe ili kujenga mahusiano mazuri na kupata ufumbuzi wa haraka kwa matatizo yaliyojitokeza.

- Jeshi la Polisi nchini ni chombo muhimu katika ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya Kisheria ili kuziba mianya inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya Kisiasa. Aidha mipango ya kuboresha utendaji kazi kitaaluma iliyopo hivi sasa upewe msukumo stahiki hususan rasilimali watu na fedha.

- Wananchi wahamasishwe kushirikiana na Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi. Polis ishirikiane na Serikali za mitaa kufanikisha malengo hayo.

- Jeshi la Polisi liimarishwe ili litekeleze majukumu yake kikamilifu na kujenga mahusiano sahihi kati yake na Jamii, Vyama vya Siasa, Tasnia ya Habari na Asasi zisizo za Kiserikali.

-Taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu unaostahiki wa upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya vyombo hivyo muhimu katika mkoa.

-Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya hatari/ghasia.

-Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi.

-Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa.

-Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.

-Viongozi wa Polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina ili zisipotoshe jamii.

-Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo na kupunguza migongano.

9.0. CHANGAMOTO

Changamoto zilizojitokeza katika Uchunguzi zimegawanyika katika mtiririko ufuatao:-

9.1 Jeshi la Polisi:

- Ukosefu wa Mafunzo endelevu.

- Ukosefu wa Uvumilivu katika utekelezaji wa Majukumu.

-Uelewa mdogo wa Elimu ya Uraia.

- Mmomonyoko wa Maadili.

- Kukosekana kwa uzalendo.

- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu

9.2 Vyama vya Siasa:

- Kukosekana kwa uvumilivu katika kuendesha shughuli za Siasa.

-Kukosekana kwa Elimu ya Uraia

- Uelewa mdogo wa baadhi ya Viongozi wa Vyama kuhusu uendeshaji wa Vyama vya Siasa.

- Ukosefu wa Sera/Mwongozo kwa Vyama vya Siasa kuendesha shughuli za Kisiasa baada ya uchaguzi mkuu.

- Kukosekana kwa Jukwaa linalokutanisha mara kwa mara Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi

- Mmomonyoko wa Maadili.

- Suala la Uzalendo.

- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu

9.3 Jamii:

- Elimu ya Uraia.

- Mmomonyoko wa Maadili.

- Kukosekana kwa uzalendo.

- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

26

10 HITIMISHO

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake aliwahi kusema kuwa, “ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Watanzania kila mtu mahali pake, tunahitaji kuwa na siasa safi yenye kujenga ustawi, tija, mshikamano, amani, maendeleo na afya kwa taifa letu”.

Utulivu na amani kwa ajili ya mustakabali wa taifa, imekuwa ni kauli mbiu ya viongozi mbalimbali ambao Kamati hii imepata fursa ya kuzungumzia juu ya hali ya siasa na mahusiano yaliyopo baina ya Serikali, (Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama wilaya na mkoa), vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi.

Wananchi na Viongozi wanataka kuona shughuli za siasa ya vyama vingi inaendeshwa kwa hoja zenye tija badala ya vurugu na utengano. Njia mojawapo ya kukabiliana na hali hii inayojitokeza ni kujenga uzalendo, maadili mema, na mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu.

Kamati hii inashauri na kupendekeza kuwa maoni haya yazingatiwe na kutekelezwa.

Aidha Kamati imefaidika sana kupata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali kuanzia kijiji hadi taifa na walitoa ushirikiano wa dhati katika kutoa mchango wao wa mawazo. Kamati inapenda kutoa shukrani za dhati kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi (Mb) kwa imani yake kwa wajumbe wa Kamati ya Uchuguzi.


the kiling ain a solution on political legitimacy

Hali ya nchini kwetu
Tanzania hadi hapa
tulipofika kwa sasa
haijalishi kuwa tunaenda
wapi mana tayari tumefika
pabaya… Kwa kundi ama
hali yoyote ile ifikapo
pabaya dawa pekee ni
suluhu ya hio hali mbaya
iliyopo iondolewe mara
moja kwa njia mbadala.
Ikumbukwe kuwa unapokuwa
na hali mbaya mara nyingi
kama sio zote HAIJALISHI
hio njia mbadala ni ipi
maadamu tu ipatikane nafuu
ya hio hali mbaya
kutoweka.
Ifikapo hali imedorola
hadi kuwa mbaya kwa
wahusika, maneno matamu na
kutia moyo hayana maana
tena! Ahadi za kuwekewa
uahueni kwa maneno
yaliyowahi tayari kutamkwa
na kujirudia kama nyimbo
za chorus hazina maana
tena! Kupozana na kupeana
pole kwa maneno ya faraja
na kusihi hakuna mana
tena! Hii yote kwa sababu
hali inapokuwa mbaya kamwe
haipati unafuu bila suluhu
ya kupunguza ama kuitoa
kabisa hio hali ambayo
kwa wakati huo tayari ni
sugu.
Mara nyingi hata magonjwa
kama vile kansa inapokuwa
imepatwa katika kiungo na
ikaonekana ni sugu ipo
njia mbili tu za kutibu;
unaua kabisa kiungo kwa
kukata kabisa kitoke ili
kisisambaze maeneo
mengine, ama unaacha na
hatima yake ni kifo cha
kutaraji ukibaki unahesabu
siku za kufa. Swali
linabaki kama unaweza
kupona kwanini ukubali
kuhesabu siku za kifo
chako?
Kwa muda mfupi sana
kumetokea vifo (ambavyo
tuna habari navyo) kwa
mkono wa Jeshi la Polisi
viwili. Ndani ya mda
mfupi vijana wawili wenye
nguvu ya kutosha kabisa
kujenga taifa letu hili
lililo sugu ya kutojengeka
wamefariki.
Tarehe 27/08/2012 Ally
Zona kafariki Morogoro
baada ya polisi kuingilia
kati maandamano yaliyokuwa
sio rasmi ya CHADEMA
kusababishia vurugu
zilizopelekea kurushwa kwa
risasi na hatimae kumpata
yeye kichwani moja wapo ya
risasi hizo, iliyopelekea
kifo cha papo hapo.
Siku 5 baadae Jana tarehe
02/09/2012 kimetokea kifo
kingine tena, safari hii
mmoja wa wanahabari
mashuhuri anaejulikana kwa
jina la David Mwangosi.
Vifo hivi vinasikitisha
sana… Natoa pole toka
moyoni kwangu kwa wafiwa
wa hao marehemu. Sie
tunalia kama taifa, wao
wanalia kuwa mtoto/baba/
kaka/mjomba na pengine
tegemezi la familia
limeyeyuka ghafla kwa njia
ambayo ingeweza kabisa
kuepushwa! Inasikitisha…
Na inauma pia.
Maswala/swali ya msingi ya
kujiuliza tokana na
matukio hayo (Na mtazamo
wangu juu ya hayo):-
Ni kweli kuwa kila vifo
vya polisi ambavo vimekuwa
vikitokea vinahusiana moja
kwa moja na CHADEMA?
Kumekuwa na misemo kwa
baadhi ya wananchi na hata
pia wanajamvi kuwa chanzo
cha vifo hivi ni vurugu
za wana CDM; labda kwa
sababu tu hizo vurugu
chanzo chake huwa uwepo
wa CDM hapo. Nabaki
najiuliza na kushangaa,
jamani watu wanapoteza
maisha lakini bado tu
hamfunguki na kutakasika
hayo macho kuona picha
halisia jinsi ilivo? Mie
nakataliana na hii Imani
kuwa CDM ndio
wanasababisha kupelekea
vifo hivo.
Wananchi wenzangu
wanaomini katika hili,
naombeni sababu za msingi
za kuamini hivo na hapo
hapo mnipe jibu kuwa wale
vijana wanao uwawa kule
migodi ya Barrick tena kwa
kulinda maslahi ya wageni
sio wazawa ni CDM
husababisha? Mnasemaje
kuhusu vifo vya vijana
watatu walio uwawa hata
wiki haijaisha kama tu
wanyama Fulani, ha hapo
hapo ni dhahiri kuwa case
closed?
Ni kweli kila itokeapo
kifo hicho kwa njia moja
ama nyingine hao marehemu
linakuwa ni kwa ajili ya
makosa yao na uzembe wao
hao marehemu?
Ingekuwa kuwa kila
wanaofariki wapo katika
kundi husika ambalo kwa
kesi hizi za vurugu ni
CDM, walau kunaweza
kukajengwa chembe ya mbegu
kichwani kuwa marehemu
alikuwa akirusha mawe na
kuletea fujo hao polisi wa
kutuliza vurugu. Inakuwaje
pale mtu ambae yupo kando
kabisa anauwawa? Hapa ni
dhahiri kabisa kuwa makosa
na uzembe (tena wa
makusudi) husukumwa na
polisi wenyewe. Ni dhahiri
pia kuwa Polisi wanakuwa
hawana umakini na kazi
yao, inakuwa kama vile
wanabahatisha tu. Kwa
kusahau wajibu wao kuwa
wao ndio tegemeo na ulinzi
wa mwananchi wa kawaida
dhidi ya lolote lile
ambalo laweza mtishia
usalama!
Katika kutuliza hizo
vurugu utumiaji wa silaha
wa polisi hulenga nini
hasa?
Ni ajabu sana, pamoja na
kusema sio polisi na sina
ujuzi huo - mimi nadhani
na ninaamini kuwa katika
taratibu za kazi kila kazi
ina namna yake ya kufanya
tokana na level ya hio
dhana inayofanyiwa kazi.
Inakuwa vipi kuwa kutuliza
vurugu kunasababishia
kutumika kwa vyombo vyo
moto moja kwa moja kwa
wananchi badala ya mbadala
kama vile angani?
Inakuwaje pale ambapo
mwananchi wa kawaida hana
silaha yoyote anauwawa
bila kifikiria hata mara
mbili? Hapa inanifanya
nitoke na hitimisho kuwa
polisi wanakuwa wamelenga
kabisa kuwa lazima
wajeruhi ama kuua mmoja
kama kukomesha/fundisho
ama kwa sababu zozote
zile walizo nazo!
Madhara ya Vifo kwa mkono
wa Polisi yanasukumwa
zaidi na muitikio kuliko
tukio lenyewe!
Maelezo na muitikio wa
Wakubwa wa Polisi
Kutokea kifo tokana na
uzembe wa kutumia silaha
kwa polisi ni swala moja,
Ila inapokuja swala la
polisi kushindwa kuvaa
kosa lao na kuwajibika
ipasavo ni KERO ambayo
kimsingi inaumiza na
kushindwa kutoa picha
kamili. Kuwa wao polisi
ni wajinga ama wanatambua
kuwa wananchi ndio
wajinga? Mfano mdogo Kifo
cha Marehemu Ally Zona
Morogoro kimeelezwa na
kamanda wa Polisi Morogoro
kuwa kilisababishwa na
kitu kizito kilichomgonga
marehemu kichwani na sio
risasi kama ilivodhaniwa…
Hii inaibua wazo na imani
kwangu kuwa; yawezekana
kabisa imesemekana hivo
ili yeyote Yule asikamatwe
kwa ajili ya kifo cha
marehemu, kuwe na kielezo
kuwa haieleweki hicho
kipande kilitoka katika
silaha ipi tofauti na
kuripoti kuwa ni risasi.
Muitikio wa Viongozi wa
juu wa Serikali
Katika hali ya kawaida
ilitakiwa viongozi
kuonesha ushirikiano hata
kwa matamko ya swala zima
lililotokea Morogoro kwa
kusababisha kifo cha huyo
kijana. Sio tu kwa msingi
wa kifo cha marehemu, ila
kwa msingi wa kusema
chama kilicho kikubwa kwa
upinzani kwa njia moja ama
nyingine kinahusika na
kufariki kwa Marehemu.
Hasa baada ya kuingilia
shughuli ambayo tayari
ilishatolewa taarifa kuwa
ipo na kutajajiwa. Kama
lipo lililosemwa basi
nimepitwa anatambua
tafadhali anijuze.
Wanachi kuchukuliwa kuwa
ni wajinga na wapumbavu!
Kwa mtitiriko na mwenendo
mzima wa jeshi la polisi
ni wazi wamechukulia kuwa
mwananchi hana haki (kwa
upande mwingine naweza
kubaliana na hii mana
jamii kwa upana haijuwi
haki zake). Kwamba
wanaweza kuvamia na kuamua
lolote hata kuua. Na
haijalishi kabisa wakiua
wanaweza eleza lolote lile
maadamu tu ionekane
wameitikia hata kama ni
kwa kusafisha jina lao ili
kuonekana wana haki ya
kufanya hivo maadamu
wanafanya kazi yao.
Marehemu kuchukuliwa kana
kwamba ni 'disposable'
Mwananchi wa kawaida na
chini amechukuliwa kama
vile mtu ambae hata haki,
hana maana,hana tija wala
umuhimu wa kulindwa.
Anaendeshwa vyovyote vile
na kupelekeshwa watakavo.
Hata hivo Polisi inatakiwa
watambue hizi ni nyakati
nyingine… Na kubwa kuliko
wananchi tumechoka! Hio
inafanya hata kumshusha
thamani huyo mwananchi
anapofariki. Jinsi
alivokufa na kuharibiwa
Marehemu David Mwamgosi,
maneno hayatoshelezi…
Inasikitisha.
Kwa mtiririko unavoenda,
kwa namna inavochukuliwa
na sharia pamoja na jeshi
la polisi ikiambatana na
serkali ni kana kwamba
vifo hivi vya kusikitisha
ni kosa lao marehemu. Kana
kwamba kufa kwao hakuna
mana wala tija, kana
kwamba ni sawa tu na kwa
namna nyingine ikicheza
kama ahadi kuwa inaweza
kutokea na HAKUNA ambalo
tunaweza kufanya.
Kwa kiasi Fulani inaweza
kuwa wapo sawa na ni
ukweli. Na hio yote
itaonesha na kudhihirishwa
na nguvu ya sisi wenyewe
wananchi kwa kuwapa nguvu
hio kwa ukimya, woga na
tabia yetu ya kutotaka
shari. Nadhani imefika
wakati wa kila mmoja wetu
kujihusisha kwa njia moja
ama nyingine kuwa kila
mmoja wetu, haijalishi upo
ndani ya chama, haijalishi
upo CDM ama CCM,
haijalishi lolote lile
zaidi ya Utambuzi, Ujuvi,
Uzalendo wa kutaka
kusongesha nchi yetu kuwa
mahala salama kwa KILA
mwananchi!
Kitu ambacho CHADEMA
wanatakiwa kujifunza:
Wamepokelewa kwa mikono
miwili na wananchi,
inatakiwa wajipange hasa.
Hizi vurugu ambazo
zimekuwa mara nyingi
zikihusishwa na wao kwa
namna moja ama nyingine
wanawajibika. Inawezekana
Serkali inafanya makusudi
kabisa ili kuwachafua kuwa
wao wanaleta fujo hadi
kusababisha vifo – Nasihi
kama mkereketwa wasafishe
hilo ili Watanzania wajue
ukweli.
Wanafanya kazi nzuri ya
kuhamasisha na kuwaamsha
wananchi kwa silaha yao ya
‘Movement for Change’. Ila
hio pekee haitoshi… Kazi,
Malengo, Mipango na nguvu
zaidi inahitajika.
Wanaweza wakawa
wamekubalika na kuzidi
kuongeza wafuasi kila
kuchapo; ila ukweli
unabaki kuwa CCM wana
mizizi mirefu hivo silaha
kubwa ya kung’oa huo
mzizi ni lazima iandaliwe
kwa Uadilifu, Umakini,
Uzalendo, Nguvu na Umoja!
Kitu ambacho CCM inatakiwa
kujifunza:
Uhakika wa kudumu kwao
katika uongozi daima wa
Serkali unazidi kupungua
kadri siku zinavoenda. Ni
wazi kuwa matatizo ya
ndani ya chama hasa
yalioendeshwa tokana na
mgawanyiko imekuwa kazi
kurekebisha. Wanachi
wamechoka na wanatambua
kila ambalo linafanywa na
serkali, kuwa hata kama
wakitaka kutokujihusisha
katika kashfa kama hizi
wanahusika moja kwa moja.
Kwa maana wakiwa kama wao
ndio tuliowapa dhamana ya
kuwa viongozi wetu,
wametuangusha na
wanatuumiza. CDM inaweza
isiwe na nguvu kama CCM,
ila kwa sasa ni dhahiri
nguvu ya Umma ipo mgongoni
kwao…
Kitu ambo Wanaharakati/
Wananchi tunatakiwa
kujifunza:
Kuongea ama kukemea
mitaani/majumbani/kwenye
vyombo vya habari pekee
HAITOSHI! We have to take
action, na action sio
lazima uende ukapigane na
mtu. Jamii yetu
imezungukwa na wananchi
ambao hawaelewi nini
kinaendelea kwa mapana
hapa nchini. Kuna ambae
ukimuuliza habari zozote
za siasa alizosikia hapa
karibuni atakujibu kwa
kujidai kabisa kuwa
“Diamond kaalikwa Ikulu”;
kwake hio ni siasa na
anakuwa kamaliza.
Nadhani imefika wakati
kama vile ambavo
ilisisitizwa kuhusu
ugonjwa wa UKIMWI kugusia
katika mkusanyiko wowote
wa watu zaidi ya watano
bila kujali ni mkutano wa
kijiwe/kazi/shughuli BASI
hata elimu ya yajirio (na
umuhimu wa kujua hayo) kwa
wanachi wenzetu iwe hivo.
Hasa wale ambao kabisaa
haelewi pa kuanzia ama
kuishia hasa kwa yale
yanayojiri nchini kwetu
kwenye hii Tanzania yetu.
Hii kelele ya mara moja
haitatibu tatizo letu
sugu… Tukitaka kutambua
kuwa na sie tuna tatizo;
tujiulize kelele zote
kuhusu Dr. Ulimboka
yakwapi? Nini kimefanyika
cha maana? Kwa mtindo huu
kweli tunadhani kunaweza
kukakwa na mabadiliko
chanya yoyote? Kwa njia
moja ama nyingine
turudishe uzalendo
tulioupoteza na kuujenga
upya…. Habari na namna
alivofariki Marehemu David
imenigusaa… Nawasilisha
hayo yote juu yakisukumwa
na hicho kifo kama moja
ya sababu.

"Usually when people are
sad, they don't do
anything. They just cry
over their condition. But
when they get angry, they
bring about change" -

Tuesday, October 2, 2012

KESI YA LEMA

UPDATES ZA MAHAKAMANI ARUSHA KWA MUJIBU WA MDAU Mungi WA MATANDAO WA JAMII FORUM

Chande: Leo waanasikiliza pingamizi za awali kwanza

Kabla hatujaanza kusikiliza, mawakili wote wawe na right of audience.

Kimomogoro: Upande wa rufani tuna uhalali wa kusimama mbele ya rufaa kwa zaidi ya miaka kumi

Alute: Nina uhalali tangu 1985

Lissu: Nimekuwa wakili tangu 2003, hivyo nina zaidi ya miaka mitano.

**************

Majaji naona wanashauriana baada ya kusikiliza maelezo ya TL kuwa ana haki ya kusikilizwa kwenye mahakama hii tukufu

Alute: Rufaa ni batili on a decree of the high court. Decree haikubaliani na hukumu.

Reference to page no 957/958 kifungu cha 14 sheria ya uchaguzi. Mkurugenzi wa uchaguzi azingatie sheria ya uchaguzi.

Decree haijaandikwa kama inavyotakiwa na sheria.

Na katika hili tumeambatanisha hukumu ya mahakama hii tukufu iliyotolewa mwezi wa tano dhidi ya Gesud Bajuta.

*************

Kesi hii imeelekeza kuwa hii decree inatakiwa iwe na format ipi. Kwenye ukurasa wa sita hadi nane.

Kwenye hii kesi tar ya decree ilikuwa imekosewa. Haya ni maelezo ya Alute yanaendelea.

Mahakama ilikumbushia umuhimu wa kuzingatia decree.

Kesi iliyopo mbele yetu decree imekosewa, haina baadhi ya maneno kama given under my hand in a seen of the court.

Decree haionyeshi ni lini imechukuliwa. Imekiuka kanuni ya tisa ya kanuni ya masijala ya mahakama.

Kanuni ya tisa "All summons shall be seen of the court. And should show when the order was distracted"

*************

Alute: Hii decree ina hitilafu, amekiri kuwa ina saini ya jaji, lakini haina muhuri wa mahakama. Bila muhuri mheshimiwa, hii decree is like a piece of paper. Decree lazima iwe kwenye formalities, na moja ya hiyo formalities ni lazima decree iwe na muhuri to show the seen of the high court. Sign peke yake haina maana.

Hii decree ni batili si makosa ya waleta rufaa bali makosa ya mahakama. Lakini pia waleta rufaa walitakiwa kuchunguza vizuri makaratasi kama yamekidhi rufaa.

Kwakuwa hii decree ni batili, basi na rufaa nayo itakuwa batili.

Chande: Alute elewa kwamba mwisho wa siku ni mambo ya mamlaka. Na aliyetoa hukumu ni jaji Rwakibarila, rufani ilisainiwa na yeye. Bado unabisha kwamba siyo mamlaka ya ofisi ya mahakama?

Alute: Bila muhuri wa mahakama the answer is no!

Chande: Kuhusu kasoro ya muda, order twenty sect. 7 haionyeshi suala la muda.

Alute: Lina uzito mheshimiwa, kwa sababu hakuna certificate of delay.

Chande anamwuliza Alute kwa maoni yake kama ameona ni batili, atoe ushauri wa adhabu mbadala.

Alute anasema kuna makosa huwa hayana adhabu mbadala.

Kweli hii kesi ya uchaguzi uchaguzi, lakini mahakama hii kwa kukosa decree of the court ilifuta kesi ya Fortunatus Machana, panga hilo hilo litumike kwenye rufaa hii.

***************
Kimomogoro:
Ningeanzia alipoishia Alute.

Anasema mwenyewe aliandika barua kuomba decree haikujibiwa. Kama yake haikujibiwa ya kwetu ingejibiwa vipi?

Mtaona kwamba drawn order imekuwa sealed. You need circumstance kusikiliza shauri hili.

Barua alizoomba corrective decree iliomba point no 4, haikuzungumzia lingine.

Msomi mwenzetu alisema marekebisho haya ili ayatumie kwenye shauri hili.

Kwa bahati mbaya barua zote hazikunukuliwa kwetu.

Msomi mwenzangu amesema hakukuwa na wajibu wa kuensure the record proper. Wakati kanuni zinamwelekeza hivyo.

Waheshimiwa tunaomba muelekeze kama mlivyomwelekeza msomi mwenzangu.

Alute hajazungumzia authorities tulizoambatanisha zinazoelezea kusahihisha decree. Tunaamini amechenga kwa makusudi

Kimomogoro:

Jukumu ni la jaji aliyetoa uamuzi kuhakikisha kuwa decree imetengenezwa. Tumetoa pia kesi ya mausi vs Arusha general store. Mahakama ilitoa mwongozo kuhusu aina ya kanuni, moja ni mandatory na directory.

Mahakama ilisisitiza kwamba kanuni za mwongozo hazitaathiri muendelezo wa kesi. Kasoro zilizotajwa kwenye hiyo zote ni clerical error.

Makosa mengine ni ya muundo 'given under my hand in a seal of the court' na date of extraction, imefutwa na GN no 6 ya mwaka jana

Mheshimiwa jaji aliridhika ni hii decree, akaweka mkono wake, kwahiyo imekamilika. Kama jaji aliridhika kimakosa, sisi hatuna makosa.

Kuhusu reg. Rule inahusika na masijala. Decree ikishapata sign ya jaji kinachofuata ni kusikilizwa.

Kama decree ni batili basi Mteja wetu bado ni mbunge wa Arusha, kwasababu hakuna kilichomtengua.....

Wednesday, August 8, 2012

TANZANIA V/S MALAWI BOUNDARIES

At around the time of independence quite a few people in Tanzania wanted to claim a huge part of Lake Malawi or Lake Nyasa . Cool heads eventually prevailed, as most Tanzanians, including the legendary President Julius Nyerere, understood the importance of respecting boundaries emanating from colonial times.

During most of Dr Kamuzu Banda’s rule, Tanzania never really pushed this crazy idea of dividing up the lake. The issue was almost forgotten during the rule of Dr Bakili Muluzi and thereafter. In fact, Dr Bingu wa Mutharika commissioned a company to start exploring oil in the lake. Tanzania said nothing at that time.

Now we have a new president and all of sudden the Tanzanians are demanding that our government stop all exploration activities in the lake until all border issues have been clarified. Why now?

Folks, there is a reason why we have tradition. Tradition may appear useless and outdated but it is important because it usually become established after a long experience. In politics there is what is known as ‘presidential protocol’. These are small things which over the years have proven to be niceties a president must or must not do in order to represent his/her country correctly.

Test for President Joyce Banda to diplomatically manage the dispute on the boundary
You would think some of them are not important but they are. Here are a few of them – presidents never bow for other presidents in public; presidents never escort anybody to their car; presidents walk with their arms spread outwards apparently projecting power and being in control; presidents usually put on a solid color (one color) necktie because it portrays power; when two presidents greet each other while facing the camera, each of them jostle to be on the right side so that his palm will face the camera- another sign of power, apparently; when in company of other presidents, they try to be the last one to enter the door – a fatherly gesture; there is an interesting video clip of Chairman Yassier Arafat and PM Ehud Barak jostling to be the last one to enter a room at Camp David. The sight of President George W Bush gently pushing PM Gordon Brown into Number 10 Downing Street before himself angered some British political experts.

Statesmanship is a game because image is everything in international politics. A country’s image depends a lot on the demeanor of its leader. President Barak Obama likes to pat other leaders on their back after greeting them; you thought that was an unplanned coincidence? Just remember, how your father used to pat you on the back when you were a good boy!

It is said that Bill Clinton failed to get a good deal at his summit with Boris Yelsin in Moscow because President Clinton having sprained his ankle arrived in Moscow on a wheelchair. The sight of a sick American president is said to have psychologically emboldened Boris Yelsin. Ghana is said to have regained its respect in West Africa when President J.J. Rawlings arrived at the 25th Organization of African Unity meeting in Togo in July 2000 in a military uniform portraying a very youthful image.

The presidency is acted on a world stage. What a president says and does is very important!

When Joyce Banda took over the presidency, she made it appear like Malawi will now be doing everything the donor community tells her to do. In fact some British newspapers were so pleasantly surprised with this that they called us ‘a donor fearing nation’.

President Joyce Banda went to London and even bowed before Queen Elizabeth, a very strange gesture considering that both are heads-of-state. Well, all these words and actions have now collectively given an image of a weak leadership in Malawi. The world has sensed blood. Now Tanzania has decided it is time to split up the lake. Notice that they did not bring up this crazy idea when Muluzi or Mutharika were in charge.

If we dignify Tanzania’s unreasonable request, one wonders what the next thing will be. Are they now going to claim Chitipa? Will Mozambique now claim Mulanje Mountain?

Government must make clear that no part of Malawi is up for discussion – full stop! It is time to show strength. Tell Tanzania that Lake Malawi was, is and will always be Malawian.

Surprisingly, after all these arrogant statements by the Tanzania government, our government’s response is at best a whimper. The minister of foreign affairs has issued a statement saying the issue will be settled ‘amicably’. Really, Mr. Minister? What could be an amicable statement? Are you planning to even dignify Tanzania’s unreasonable demand? Do you plan to divide up the lake? How can you have an amicable settlement to an unreasonable demand?

Thursday, July 5, 2012

JE, TUNAUJUA UKWELI JUU YA MUUNGANO? HII NI HOTUBA YAB MH. TUNDU LISSU

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO),
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2012/2013
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,

Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza miaka arobaini na nane tangu kuzaliwa kwake baada ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika Mwalimu Nyerere kutia saini Makubaliano ya Muungano na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Sheikh Abedi Amani Karume tarehe 22 Aprili, 1964.

Wakati anawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) aliliambia Bunge lako tukufu kwamba “... katika kipindi hicho Muungano wetu umekuwa na mafanikio katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.... Muungano wetu ndio nguzo kuu ya umoja na amani.”

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aliliambia Bunge lako tukufu kwamba, licha ya mafanikio hayo, “... zipo changamoto katika kumaliza vikwazo vinavyokwamisha shughuli za Muungano.” Mheshimiwa Waziri hakuzitaja changamoto hizo.

‘MAPITO’ YA MUUNGANO

Mheshimiwa Spika,

Katika Utangulizi wake kwa Chapisho la Pili la Mhadhara wa Kiprofesa (Professorial Inaugural Lecture) uliotolewa Januari 1990 na Profesa Issa G. Shivji na kupewa kichwa cha Tanzania: The Legal Foundations of the Union, Profesa Yash Ghai - aliyekuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa kwanza kutoka Afrika Mashariki - anasema kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kuanzishwa kwa Muungano na historia yake, “... kitu cha ajabu sio kwamba umekuwa na matatizo, bali ni kwamba umedumu (licha ya matatizo hayo) – na kwenda kinyume na mwelekeo katika Afrika.”

Muungano ulidumu misuguano ya miaka ya mwanzo kati ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume iliyohusu kuongezwa kwa masuala ya fedha na sarafu katika orodha ya Mambo ya Muungano. Aidha, Muungano ulidumu mauaji ya viongozi waandamizi na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Abdallah Kassim Hanga, Waziri wa Fedha Abdul Aziz Twala, Othman Sharrif, Mdungi Ussi, Saleh Saadalla na wengine wengi.

Vile vile, Muungano ulidumu mauaji ya Sheikh Karume mwenyewe mwaka 1972; ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar iliyopelekea kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe mwaka 1984; alichokiita Mwalimu Nyerere ‘udhaifu’ wa Rais Mwinyi; na kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka 1999.

Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Spika, ‘mapito’ haya ya Muungano yamekuwa yanafichwa fichwa, licha ya kauli za mara kwa mara za ‘kuelimisha umma juu ya Muungano.’ Kwa sababu hiyo, zaidi ya tendo la kuchanganya udongo na matukio mengine yaliyofanyika hadharani, historia halisi ya Muungano wetu haifahamiki kwa wananchi walio wengi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba wakati umefika sasa kwa Serikali kuweka wazi nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya Muungano wetu na ‘mapito’ yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea yanayouhusu.

Hii ni muhimu zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika katika kuzaliwa kwa Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbali mbali za Serikali kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za nchi hizo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za kibeberu za kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar la wakati huo.

Aidha, nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano inabaki pungufu. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, miaka karibu hamsini ya Muungano ni umri wa kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.

UKIUKWAJI MAKUBALIANO/SHERIA YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,

Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili 1964 yalikuwa ni mkataba wa kimataifa kati ya nchi mbili huru zilizokubaliana kuunda ‘nchi moja huru’, kwa mujibu wa ibara ya (i) ya Hati ya Muungano. Ili kutekeleza Makubaliano ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Tanganyika lilitunga Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania. Kifungu cha 4 cha Sheria hiyo kilitangaza kuunganishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa ‘Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’

Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la Mapinduzi – ambalo ndio lilikuwa ‘Bunge’ la Zanzibar wakati huo – halikutunga sheria ya kuridhia Makubaliano ya Muungano. Jambo hili limekuwa chanzo cha mjadala mkali katika duru za kitaaluma na kisheria juu ya uhalali wa Muungano wenyewe. Kwa vyovyote vile, matokeo ya kusainiwa Makubaliano ya Muungano ni kwamba Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikufa na nchi moja – iliyokuja baadae kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - kuzaliwa.

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa aya ya (iv) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Muungano, Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa kwenye Makubaliano ya Muungano yalikuwa kumi na moja. Haya ni mambo yaliyoko katika vipengele vya 1 hadi 11 vya Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Muungano. Hata hivyo, kati ya mwaka 1964 and 1973 mambo mengine sita – yanayoonekana katika vipengele 12 hadi 16 vya Nyongeza ya Kwanza – yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Hivyo basi, mwaka 1965 masuala ya fedha, sarafu na benki yaliongezwa; mwaka 1967 leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu na mambo yaliyokuwa katika Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa; mwaka 1968 yaliongezwa mambo ya maliasili ya mafuta, petroli na gesi asilia; na mwaka 1973 mambo yanayohusu Baraza la Mitihani la Taifa yaliongezwa.

Aidha, Mheshimiwa Spika, Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya mwaka 1984 yaligawa kipengele cha Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutengeneza vipengele vinne vinavyojitegemea katika orodha ya Mambo ya Muungano, yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa hali ya hewa na takwimu.

Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu kipya katika orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, kipengele cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho na kuwa ‘ulinzi na usalama.’ Na mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya siasa’ nao uliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Mambo yote yaliyoongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano baada ya mwaka 1964 yalikuwa nje ya Makubaliano ya Muungano na nje ya Sheria ya Muungano na kwa hiyo yalikuwa batili. Hii ni kwa sababu Sheria ya Muungano – na sio Katiba za Muda za 1964 au 1965 au ya sasa - ndio Sheria Mama iliyozaa Muungano na kuweka mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka za Jamhuri ya Muungano na mamlaka za Zanzibar. Sheria ya Muungano ilitungwa na Bunge la Katiba tofauti na sheria za kawaida.

Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala Tanzania hadi 1977 iliiweka Sheria hiyo kama Nyongeza ya Pili katika Katiba na kuweka masharti kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa bila marekebisho hayo kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanganyika na wale wa Zanzibar. Vile vile, Katiba ya Muunganoinataja, katika Orodha ya Kwanza ya Nyongeza ya Pili, kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake yahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote ni “Sura ya 557 (Toleo la 1965), Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.”

Mambo yote haya, Mheshimiwa Spika, yanaifanya Sheria ya Muungano kuwa na haiba ya Katiba. Kama alivyosema Profesa Issa Shivji katika The Legal Foundations of the Union: “Kila mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sheria amefundishwa kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapatikana katika waraka unaoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Lakini, nachelea kusema, kila mwanafunzi amefundishwa visivyo.

Katiba ya Tanzania inapatikana sio katika waraka mmoja, bali katika nyaraka mbili. Sheria ya Muungano, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania na Sheria ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.... Vivyo hivyo, Katiba ya Zanzibar inapatikana katika (1) Sheria ya Muungano na (2) Katiba ya Zanzibar, 1984.” Katika masuala yanayohusu Muungano, kwa mujibu wa Profesa Shivji, waraka unaotawala ni Sheria ya Muungano.

Hii ndio kusema kwamba panapotokea mgongano kati ya Katiba au Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Muungano, ni Sheria ya Muungano ndio inayokuwa na Katiba au Katiba ya Zanzibar inakuwa batili kwa kiasi cha ukiukaji wake wa Sheria ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kifungu cha 5 cha Sheria ya Muungano, ambacho ndicho chenye misingi mikuu ya Muungano hakijawahi kurekebishwa tangu Sheria yenyewe ilipotungwa mwaka 1964. Badala yake, Bunge limekuwa na tabia ya kukwepa kuigusa kabisa Sheria ya Muungano na badala yake limekuwa likifanya marekebisho ya orodha ya Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika Katiba za Muda za mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza vipengele katika orodha hiyo. Lengo la marekebisho haya, Mheshimiwa Spika, limekuwa mara zote ni kuinyang’anya Zanzibar mamlaka yake chini ya Sheria ya Muungano.

Ndio maana katika Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyotolewa tarehe 27 Januari, 1983, CCM ilitamka kwamba “... msingi wa kuwa na orodha ya mambo ya muungano katika Katiba ni kuonyesha mamlaka ya Serikali ya Zanzibar ambayo yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano; na msingi wa kuongeza mambo zaidi katika orodha ya mambo ya muungano, kama ambavyo imefanyika mara kwa mara, ni kuhamisha mamlaka zaidi ya Serikali ya Zanzibar kwenda kwa Serikali ya Muungano.”

Mheshimiwa Spika,

Profesa Shivji anasema - katika The Legal Foundations of the Union - kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa mamlaka ya kuongeza Mambo ya Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu Mambo ya Muungano kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya Muungano. Kwa maana hiyo, nyongeza zote zilizofanyika katika orodha ya Mambo ya Muungano tangu mwaka 1964 zilikiuka Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano na ni batili. Ndio maana, kwa muda mrefu, Wazanzibari wamelalamikia masuala haya, hasa hasa masuala ya fedha, sarafu na mafuta na gesi asilia.

Mheshimiwa Spika,

Vitendo vya kupuuza Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano vilifikia kilele chake tarehe 21 Novemba, 2000 pale Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilipotamka – katika kesi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 – kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani, ‘hakuna ubishi wa aina yoyote kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi moja na dola moja.’

Kama tulivyokwisha kuonyesha, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania yenyewe kuwa suala la Muungano liliingizwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kinyemela na kinyume na Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano. Jibu la Wazanzibari juu ya ukiukwaji wa muda mrefu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010.

KATIBA YA MUAFAKA AU KATIBA YA UHURU?
Mheshimiwa Spika,

Misukosuko ambayo imeukumba Muungano wetu tangu mwaka 1964 hailingani na hatari kubwa inayoukabili hivi sasa. Kama tulivyomweleza Rais Kikwete katika waraka wetu wa tarehe 27 Novemba, 2011, “Muungano wetu upo katika hatari kubwa ya kuvunjika kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya kikatiba ambayo yamefanyika katika Katiba ya Zanzibar, 1984 na kutokana na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Hii ni kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba, 2010, inaashiria tafsiri mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inahoji misingi ya Jamhuri ya Muungano kama nchi moja, mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, na mambo muhimu ya Muungano....” Ili kufahamu jambo hili vizuri, ni muhimu kuelewa kwa undani yaliyomo katika Sheria hiyo ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,

Tarehe 13 Agosti, 2010, wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa limevunjwa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka msingi wa kikatiba wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha CCM na Chama cha Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imepigiwa upatu kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni kweli.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji uhalali wa orodha ya Mambo ya Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza zake zilizofuata, bali pia imehoji pia misingi muhimu ya Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huu, Katiba ya sasa ya Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi kuliko waraka wa muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa mahasimu.

Mheshimiwa Spika,
Aya ya (i) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano vilitangaza muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa ‘Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’

Huu ndio msingi wa maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Muungano kwamba ‘Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.’ Na huu ndio ulikuwa msingi wa maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar ya kabla ya Mabadiliko ya 2010 kwamba ‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.’ Sasa msingi huu wa Muungano umehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba mpya ya Zanzibar yanayotamka kwamba ‘Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’

Mheshimiwa Spika,

Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano – kwa kushauriana kwanza na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo. Vile vile, ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Zanzibar mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya kushauriana na Rais.’ Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na mamlaka za mikoa hiyo sio, na hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano.

Vile vile hayapo katika orodha ya Mambo ya Muungano. Ni wazi kwa hiyo, kwamba ibara za 2(2) na 61(3) za Katiba ya Muungano zilikuwa zinakiuka matakwa ya Sheria ya Muungano na kwa hiyo ni batili. Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia uhuru’ kwa kutangaza – katika ibara ya 2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba “... Rais (wa Zanzibar) aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.” Aidha, kwa ibara ya 61(1), Rais wa Zanzibar hawajibiki tena kushauriana na Rais wa Muungano pale anapofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Wakati ambapo Sheria ya Muungano ilikuwa imetambua na kuhifadhi mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama mkuu wa dola ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – katika Kesi ya Machano Khamis Ali na Wenzake – ilitishia moja kwa moja msingi huo kwa kutamka kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola na kwa hiyo haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini.

Sasa ibara ya 26(1) ya Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha’ dola ya Zanzibar kwa kutamka kwamba “kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.” Aidha, kwa kutambua kwamba ‘Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano’ sio moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar imetamka kwamba katika kesi zinazohusu ‘kinga za haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi’, uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar “... utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.”

Mheshimiwa Spika,

Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya Muungano kinataja ‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo kumi na moja ya Muungano. Na hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya Muungano. Ijapokuwa ‘ulinzi’ ulichakachuliwa baadae kwa kuongezwa maneno ‘na usalama’, bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi na polisi ni masuala halali ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali ya Muungano.

Na kwa sababu hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya Muungano kutamka – kama inavyofanya katika ibara ya 33(2) - kwamba ‘Rais (wa Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.’

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, katika kile kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.’

Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya 121(2) ni Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Chuo cha Mafunzo (cha wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo Rais wa Zanzibar anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa....’ Kuthibitisha kwamba Idara Maalum ni majeshi, ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum ‘... kujishughulisha na mambo ya siasa....’ Makatazo haya hayatofautiani na makatazo ya wanajeshi kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika ibara ya 147(3) ya Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Sio tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar inaanzisha majeshi bali pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa Kamanda Mkuu wa Idara Maalum na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa.” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1) yanaingiza “... uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli yoyote inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya Taifa.”

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haya ni mamlaka ya kutangaza au kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hii ya ibara ya 123 ya Katiba mpya ya Zanzibar ni sahihi.

Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tamko Bungeni ni kwa nini imeiruhusu Zanzibar kujinyakulia mamlaka juu ya mambo ya ulinzi na usalama ambayo kwa historia yote ya Muungano yamekuwa ni mamlaka pekee ya Serikali ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Muungano kilitamka kwamba muundo wa Serikali ya Zanzibar utakuwa kama utakavyoamuliwa na sheria za Zanzibar pekee. Na hivyo ndivyo ilivyokubaliwa katika aya ya (iii)(a) ya Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo wa Serikali ya Zanzibar kutokuwepo katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba ya Muungano imetenga Sura ya Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’

Kwa mujibu wa Profesa Shivji katika The Legal Foundations of the Union, Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano “... haina ulazima wowote na ni kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako ndani ya mamlaka pekee ya Zanzibar.” Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar – kwa usahihi kabisa - imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Katiba mpya ya Zanzibar sio tu kwamba ‘imetangaza uhuru’ wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu ya Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano, bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote la Serikali ya Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwepo kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa mujibu wa ibara ya 80A(1) ya Katiba hiyo, “... Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba kuhusiana na sharti lolote lililomo katika kifungu chochote kilichoainishwa katika kijifungu cha (2) cha kifungu hiki, mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.”

Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu vyote vya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au dola; kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka yake.

Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana nayo.

Mheshimiwa Spika,

Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari.

Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala ya kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku, Mheshimiwa Spika, ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru! Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani!

Mheshimiwa Spika,

Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, hatuna tena nchi moja inayozungumzwa katika Katiba ya Muungano bali tuna nchi mbili. Kwa mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena Mambo ya Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi wawili viongozi wa serikali wawili. Haya yote yanakiuka moja kwa moja Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.

Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Muungano - haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar. Yote haya hayapo katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano lakini yapo katika Katiba ya Muungano.

KURUDISHWA KWA SERIKALI YA TANGANYIKA

Mheshimiwa Spika,

Katika maoni yetu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha jinsi ambavyo “tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetiliwa nguvu kubwa na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imeipa Zanzibar nafasi na ushawishi mkubwa katika utungaji wa Katiba Mpya.”

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha kwamba, kwa mujibu wa Sheria hiyo, “Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya turufu katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.” Aidha, tulithibitisha jinsi ambavyo “... ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake (bali) Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vingine vinavyoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba....”

Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia tena tahadhari iliyoitoa wakati huo kwamba: “Masharti haya ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana athari kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu yanakiuka Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na hata Katiba ya sasa ya Zanzibar....” Na kama tulivyosema wakati huo, “... tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inarudisha mezani mjadala juu ya muundo wa Muungano wetu na nafasi ya iliyokuwa Tanganyika katika Muungano huo.”

Mheshimiwa Spika,

Kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru kama ambavyo tumeonyesha hapa, huu ni wakati muafaka kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika.

Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano sio tu una Serikali kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya. Katika mazingira kama haya, Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na vitu vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika hali ya usawa.

Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama Kimoja au Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama ilivyopendekezwa na Kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!

KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaielekeza Tume ya Katiba kuongozwa na misingi mikuu ya kitaifa ya kuhifadhi na kudumisha ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano.’ Hata hivyo, baada ya kujitokeza kwa wananchi wanaopinga kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba amesema kwamba wale wanaopinga Muungano nao wajitokeze kutoa maoni yao kwa Tume.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu ni namna gani maoni ya wale wanaotaka kiini macho hiki cha Muungano kiishe yatashughulikiwa na Tume ambayo imepewa jukumu kisheria la kukihifadhi na kukidumisha kiini macho hicho? Ni kipi kitakachoizuia Tume ya Warioba kupuuza maoni ya watu hao kwa hoja kwamba Sheria inaielekeza Tume kuratibu na kukusanya maoni na kutoa mapendekezo ya kuhifadhi na kudumisha Muungano?
Mheshimiwa Spika,

Katika miezi ya karibuni kumejitokeza makundi ya wananchi, hasa kwa upande wa Zanzibar, ambayo yamedai kwamba iitishwe kura ya maoni ya wananchi ili kuamua kama bado kuna haja ya kuendelea na Muungano. Makundi haya, yakiongozwa na kundi la Uamsho, yameshambuliwa sana hadharani kwa kudaiwa kwamba yanataka kuvunja Muungano. Na watu ambao wameongoza mashambulizi dhidi ya wana-Uamsho ni viongozi waandamizi wa CCM, wakiwemo viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho.

Mheshimiwa Spika,

Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulisema kwamba “... hofu ... ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano - juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010.” Naomba nikiri kwamba tulikosea kusema hivyo.

Tulichotakiwa kusema wakati ule, na tunachokisema sasa, ni kwamba kimya kikuu ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya ukiukwaji mkubwa wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano pamoja na Katiba kinatokana sio tu na ‘hofu’ ya kuwaudhi Wazanzibari bali pia kinatokana na ukweli kwamba viongozi waandamizi wa CCM pamoja na wa Serikali yake walishiriki katika ukiukwaji huo!

Wao ndio wanaoongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio waliondaa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar. Na wao ndio wanaoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliokula kiapo cha kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kwa hiyo wao ndio walioiruhusu Zanzibar kutangaza uhuru kwa Mabadiliko haya ya Katiba yake.

Mheshimiwa Spika,

Kwa viongozi hawa na chama chao kuibuka sasa na kuwatuhumu wana-Uamsho na makundi mengine kwamba wanataka kuvunja Muungano kwa kudai kura ya maoni ya wananchi wakati wao wenyewe wamekaa na kupitisha marekebisho ya Katiba ambayo tayari yamevunja Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano ni kilele cha juu cha unafiki wa kisiasa. Mashabiki hawa wa Muungano waeleze walikuwa wapi wakati Zanzibar inatangaza uhuru wake kwa kuchanachana Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kwa wale wanaodai kwamba wana-Uamsho wanataka kuvunja Muungano kwa sababu tu ya kudai kura ya maoni, tunaomba tuwakumbushe yafuatayo. Kwanza, kwa mujibu wa Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa.”

Hapa Mwalimu alikuwa anamzungumzia aliyekuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy waliong’olewa madarakani mwaka 1984 baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa.’

Aidha, Mheshimiwa Spika, katika kitabu hicho hicho Mwalimu Nyerere anasema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge hili hili wakati wa Bunge la bajeti la mwaka 1993: “Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai (kwamba) kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano....

Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya Tanganyika’ ndani ya Muungano.... Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine ... iliyokuwa inalitaka Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano....”

Pili, Mheshimiwa Spika, Katiba ya sasa ya Zanzibar ambayo mashabiki wa Muungano wameileta kwa kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba tayari imewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kuamua, kwa kura ya maoni, mambo mbali mbali yanayoihusu nchi hiyo na namna itakavyoongozwa. Mashabiki hawa wa Muungano wakubali kuvuna walichopanda, wasibeze wale wote wanaotaka kutumia haki ya kura ya maoni kuamua hatma ya Muungano na nafasi ya Zanzibar ndani au nje yake.

Mheshimiwa Spika,

Ni wazi, kwa kuzingatia ushahidi huu, kwamba madai ya kuwa na kura ya maoni ya wananchi ili kuamua masuala makubwa yanayohusu Muungano wetu ni ya siku nyingi na yametolewa na watu na taasisi mbali mbali. Madai haya hayajaanzishwa na wana-Uamsho wala CHADEMA. Ni wazi vile vile kwamba kura ya maoni inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar.

Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wale wote ambao wamedai, na wanaendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakbala wa nchi yetu. Kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati Serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja kivitendo kutaipelekea nchi yetu kwenye njia ya Ethiopia na Eritrea, au Sudan na Sudan Kusini au Yugoslavia ya zamani.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni ndio, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne ya Muungano inatosha basi itakuwa afadhali kwenda njia ya Czechoslovakia ya zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au Ethiopia na Eritrea au Sudan na Sudan Kusini.

Mwisho, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania juu ya hatua, kama zipo, ilizozichukua kuzuia ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba. Na mwisho, Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama - kwa ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano – Bunge hili tukufu litakuwa ndani ya mamlaka yake kuchukua hatua za kumshtaki Rais kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba kwa kushindwa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Muungano kama kiapo cha kazi yake kinavyomtaka.

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano uliowezesha maandalizi ya maoni haya. Aidha, niwashukuru familia yangu – mke wangu mpenzi Alicia Bosensera na mapacha wetu Agostino Lissu na Edward Bulali – kwa kuendelea kuvumilia upweke unaotokana na ‘Daddy’ kuwa mbali muda mwingi kwa sababu ya majukumu mazito ya kibunge.

Aidha, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida Mashariki kwa imani na nguvu wanayonipa kila siku kwa kuendeleza msimamo wetu thabiti wa kukataa kunyanyaswa, kunyonywa na kupuuzwa na ‘Ndaa ya Njou’! Mwisho naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama na wapenzi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote wa Tanzania ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu. Ninawaomba waendelee kutuunga mkono na kututia nguvu katika siku ngumu na za majaribu makubwa zinazokuja!

Mheshimiwa Spika,

Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.

---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI