JE, TUNAUJUA UKWELI JUU YA MUUNGANO? HII NI HOTUBA YAB MH. TUNDU LISSU
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO),
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2012/2013
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza miaka
arobaini na nane tangu kuzaliwa kwake baada ya Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika Mwalimu Nyerere kutia saini Makubaliano ya Muungano na Rais
wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Sheikh Abedi Amani Karume tarehe 22
Aprili, 1964.
Wakati anawasilisha Makadirio ya Mapato
na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Mheshimiwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) aliliambia Bunge lako tukufu kwamba
“... katika kipindi hicho Muungano wetu umekuwa na mafanikio katika
maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.... Muungano wetu ndio nguzo kuu
ya umoja na amani.”
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa Waziri aliliambia Bunge lako tukufu kwamba, licha ya
mafanikio hayo, “... zipo changamoto katika kumaliza vikwazo
vinavyokwamisha shughuli za Muungano.” Mheshimiwa Waziri hakuzitaja
changamoto hizo.
‘MAPITO’ YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika Utangulizi wake kwa Chapisho la Pili la Mhadhara wa
Kiprofesa (Professorial Inaugural Lecture) uliotolewa Januari 1990 na
Profesa Issa G. Shivji na kupewa kichwa cha Tanzania: The Legal
Foundations of the Union, Profesa Yash Ghai - aliyekuwa Mkuu wa Kitivo
cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa kwanza kutoka Afrika
Mashariki - anasema kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kuanzishwa kwa
Muungano na historia yake, “... kitu cha ajabu sio kwamba umekuwa na
matatizo, bali ni kwamba umedumu (licha ya matatizo hayo) – na kwenda
kinyume na mwelekeo katika Afrika.”
Muungano ulidumu
misuguano ya miaka ya mwanzo kati ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume
iliyohusu kuongezwa kwa masuala ya fedha na sarafu katika orodha ya
Mambo ya Muungano. Aidha, Muungano ulidumu mauaji ya viongozi waandamizi
na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza la Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Abdallah
Kassim Hanga, Waziri wa Fedha Abdul Aziz Twala, Othman Sharrif, Mdungi
Ussi, Saleh Saadalla na wengine wengi.
Vile vile,
Muungano ulidumu mauaji ya Sheikh Karume mwenyewe mwaka 1972; ‘kuchafuka
kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar iliyopelekea kung’olewa
madarakani kwa Rais Aboud Jumbe mwaka 1984; alichokiita Mwalimu Nyerere
‘udhaifu’ wa Rais Mwinyi; na kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka 1999.
Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Spika, ‘mapito’ haya ya Muungano
yamekuwa yanafichwa fichwa, licha ya kauli za mara kwa mara za
‘kuelimisha umma juu ya Muungano.’ Kwa sababu hiyo, zaidi ya tendo la
kuchanganya udongo na matukio mengine yaliyofanyika hadharani, historia
halisi ya Muungano wetu haifahamiki kwa wananchi walio wengi. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba wakati umefika sasa kwa
Serikali kuweka wazi nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya Muungano
wetu na ‘mapito’ yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea
yanayouhusu.
Hii ni muhimu zaidi kwa kuzingatia ukweli
kwamba mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza
yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na
balozi zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa
hayo zilihusika katika kuzaliwa kwa Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbali mbali za
Serikali kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo
chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za nchi hizo kwamba
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za kibeberu za
kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na
viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar la wakati huo.
Aidha, nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu
viongozi waandamizi wa chama hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa
rasmi, historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano inabaki pungufu.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, miaka karibu hamsini ya
Muungano ni umri wa kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote
juu ya kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.
UKIUKWAJI MAKUBALIANO/SHERIA YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili 1964 yalikuwa ni
mkataba wa kimataifa kati ya nchi mbili huru zilizokubaliana kuunda
‘nchi moja huru’, kwa mujibu wa ibara ya (i) ya Hati ya Muungano. Ili
kutekeleza Makubaliano ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Tanganyika
lilitunga Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, Sura ya
557 ya Sheria za Tanzania. Kifungu cha 4 cha Sheria hiyo kilitangaza
kuunganishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
kuwa ‘Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar.’
Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la
Mapinduzi – ambalo ndio lilikuwa ‘Bunge’ la Zanzibar wakati huo –
halikutunga sheria ya kuridhia Makubaliano ya Muungano. Jambo hili
limekuwa chanzo cha mjadala mkali katika duru za kitaaluma na kisheria
juu ya uhalali wa Muungano wenyewe. Kwa vyovyote vile, matokeo ya
kusainiwa Makubaliano ya Muungano ni kwamba Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikufa na nchi moja – iliyokuja baadae
kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - kuzaliwa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa aya ya (iv) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu
cha 5(1) cha Sheria ya Muungano, Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa
kwenye Makubaliano ya Muungano yalikuwa kumi na moja. Haya ni mambo
yaliyoko katika vipengele vya 1 hadi 11 vya Nyongeza ya Kwanza ya Katiba
ya Muungano. Hata hivyo, kati ya mwaka 1964 and 1973 mambo mengine sita
– yanayoonekana katika vipengele 12 hadi 16 vya Nyongeza ya Kwanza –
yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Hivyo
basi, mwaka 1965 masuala ya fedha, sarafu na benki yaliongezwa; mwaka
1967 leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu na mambo yaliyokuwa
katika Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
yaliongezwa; mwaka 1968 yaliongezwa mambo ya maliasili ya mafuta,
petroli na gesi asilia; na mwaka 1973 mambo yanayohusu Baraza la
Mitihani la Taifa yaliongezwa.
Aidha, Mheshimiwa Spika,
Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya mwaka 1984 yaligawa kipengele cha
Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutengeneza
vipengele vinne vinavyojitegemea katika orodha ya Mambo ya Muungano,
yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa hali ya hewa
na takwimu.
Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu
kipya katika orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya
Tanzania. Aidha, kipengele cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho
na kuwa ‘ulinzi na usalama.’ Na mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya
siasa’ nao uliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Mambo yote yaliyoongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano
baada ya mwaka 1964 yalikuwa nje ya Makubaliano ya Muungano na nje ya
Sheria ya Muungano na kwa hiyo yalikuwa batili. Hii ni kwa sababu Sheria
ya Muungano – na sio Katiba za Muda za 1964 au 1965 au ya sasa - ndio
Sheria Mama iliyozaa Muungano na kuweka mgawanyo wa madaraka kati ya
mamlaka za Jamhuri ya Muungano na mamlaka za Zanzibar. Sheria ya
Muungano ilitungwa na Bunge la Katiba tofauti na sheria za kawaida.
Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala Tanzania hadi 1977
iliiweka Sheria hiyo kama Nyongeza ya Pili katika Katiba na kuweka
masharti kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa bila marekebisho hayo
kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanganyika na wale wa
Zanzibar. Vile vile, Katiba ya Muunganoinataja, katika Orodha ya Kwanza
ya Nyongeza ya Pili, kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake
yahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote ni “Sura ya 557
(Toleo la 1965), Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.”
Mambo yote haya,
Mheshimiwa Spika, yanaifanya Sheria ya Muungano kuwa na haiba ya
Katiba. Kama alivyosema Profesa Issa Shivji katika The Legal Foundations
of the Union: “Kila mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sheria
amefundishwa kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inapatikana katika waraka unaoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977. Lakini, nachelea kusema, kila mwanafunzi amefundishwa
visivyo.
Katiba ya Tanzania inapatikana sio katika
waraka mmoja, bali katika nyaraka mbili. Sheria ya Muungano, Sura ya 557
ya Sheria za Tanzania na Sheria ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.... Vivyo hivyo, Katiba ya Zanzibar inapatikana katika (1)
Sheria ya Muungano na (2) Katiba ya Zanzibar, 1984.” Katika masuala
yanayohusu Muungano, kwa mujibu wa Profesa Shivji, waraka unaotawala ni
Sheria ya Muungano.
Hii ndio kusema kwamba panapotokea
mgongano kati ya Katiba au Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Muungano, ni
Sheria ya Muungano ndio inayokuwa na Katiba au Katiba ya Zanzibar
inakuwa batili kwa kiasi cha ukiukaji wake wa Sheria ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Muungano, ambacho ndicho chenye
misingi mikuu ya Muungano hakijawahi kurekebishwa tangu Sheria yenyewe
ilipotungwa mwaka 1964. Badala yake, Bunge limekuwa na tabia ya kukwepa
kuigusa kabisa Sheria ya Muungano na badala yake limekuwa likifanya
marekebisho ya orodha ya Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa mara ya kwanza
katika Katiba za Muda za mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza vipengele
katika orodha hiyo. Lengo la marekebisho haya, Mheshimiwa Spika,
limekuwa mara zote ni kuinyang’anya Zanzibar mamlaka yake chini ya
Sheria ya Muungano.
Ndio maana katika Mapendekezo ya
Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyotolewa tarehe
27 Januari, 1983, CCM ilitamka kwamba “... msingi wa kuwa na orodha ya
mambo ya muungano katika Katiba ni kuonyesha mamlaka ya Serikali ya
Zanzibar ambayo yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano; na msingi wa
kuongeza mambo zaidi katika orodha ya mambo ya muungano, kama ambavyo
imefanyika mara kwa mara, ni kuhamisha mamlaka zaidi ya Serikali ya
Zanzibar kwenda kwa Serikali ya Muungano.”
Mheshimiwa Spika,
Profesa Shivji anasema - katika The Legal Foundations of the
Union - kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa mamlaka ya
kuongeza Mambo ya Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria
zinazohusu Mambo ya Muungano kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya
Muungano. Kwa maana hiyo, nyongeza zote zilizofanyika katika orodha ya
Mambo ya Muungano tangu mwaka 1964 zilikiuka Makubaliano ya Muungano na
Sheria ya Muungano na ni batili. Ndio maana, kwa muda mrefu, Wazanzibari
wamelalamikia masuala haya, hasa hasa masuala ya fedha, sarafu na
mafuta na gesi asilia.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo vya kupuuza Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano
iliyoridhia Makubaliano vilifikia kilele chake tarehe 21 Novemba, 2000
pale Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilipotamka – katika kesi ya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 –
kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama
ya Rufani, ‘hakuna ubishi wa aina yoyote kwamba Jamhuri ya Muungano ni
nchi moja na dola moja.’
Kama tulivyokwisha kuonyesha,
suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania yenyewe kuwa suala la Muungano
liliingizwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kinyemela na kinyume na
Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano. Jibu la Wazanzibari juu
ya ukiukwaji wa muda mrefu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya
Muungano iliyoridhia Makubaliano hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya
Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010.
KATIBA YA MUAFAKA AU KATIBA YA UHURU?
Mheshimiwa Spika,
Misukosuko ambayo imeukumba Muungano wetu tangu mwaka 1964
hailingani na hatari kubwa inayoukabili hivi sasa. Kama tulivyomweleza
Rais Kikwete katika waraka wetu wa tarehe 27 Novemba, 2011, “Muungano
wetu upo katika hatari kubwa ya kuvunjika kwa sababu ya mabadiliko
makubwa ya kikatiba ambayo yamefanyika katika Katiba ya Zanzibar, 1984
na kutokana na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hii ni kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba, 2010,
inaashiria tafsiri mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inahoji misingi ya Jamhuri ya
Muungano kama nchi moja, mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, na
mambo muhimu ya Muungano....” Ili kufahamu jambo hili vizuri, ni muhimu
kuelewa kwa undani yaliyomo katika Sheria hiyo ya Mabadiliko ya Kumi ya
Katiba Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe
13 Agosti, 2010, wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa limevunjwa
kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Baraza la Wawakilishi
la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya
Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka msingi wa kikatiba wa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha CCM na Chama cha
Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
imepigiwa upatu kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni
kweli.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji
uhalali wa orodha ya Mambo ya Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza
zake zilizofuata, bali pia imehoji pia misingi muhimu ya Sheria ya
Muungano iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huu, Katiba ya
sasa ya Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi
kuliko waraka wa muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa mahasimu.
Mheshimiwa Spika,
Aya ya (i) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 4 cha
Sheria ya Muungano vilitangaza muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa ‘Jamhuri moja huru
itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Huu ndio msingi wa maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Muungano
kwamba ‘Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.’ Na huu ndio
ulikuwa msingi wa maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar ya kabla ya
Mabadiliko ya 2010 kwamba ‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.’
Sasa msingi huu wa Muungano umehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba
mpya ya Zanzibar yanayotamka kwamba ‘Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili
zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Jamhuri ya
Muungano – kwa kushauriana kwanza na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya
kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo. Vile
vile, ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Zanzibar
mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya
kushauriana na Rais.’ Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na
mamlaka za mikoa hiyo sio, na hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa
mujibu wa Sheria ya Muungano.
Vile vile hayapo katika
orodha ya Mambo ya Muungano. Ni wazi kwa hiyo, kwamba ibara za 2(2) na
61(3) za Katiba ya Muungano zilikuwa zinakiuka matakwa ya Sheria ya
Muungano na kwa hiyo ni batili. Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia uhuru’
kwa kutangaza – katika ibara ya 2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba
“... Rais (wa Zanzibar) aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na
maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa
na Baraza la Wawakilishi.” Aidha, kwa ibara ya 61(1), Rais wa Zanzibar
hawajibiki tena kushauriana na Rais wa Muungano pale anapofanya uteuzi
wa wakuu wa mikoa ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Wakati ambapo Sheria ya Muungano ilikuwa imetambua na kuhifadhi
mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama mkuu wa dola ya Zanzibar, Mahakama ya
Rufani ya Tanzania – katika Kesi ya Machano Khamis Ali na Wenzake –
ilitishia moja kwa moja msingi huo kwa kutamka kwamba Zanzibar sio nchi
na wala sio dola na kwa hiyo haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini.
Sasa ibara ya 26(1) ya Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha’ dola
ya Zanzibar kwa kutamka kwamba “kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye
atakuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.” Aidha, kwa kutambua kwamba
‘Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano’ sio moja ya Mambo ya
Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar
imetamka kwamba katika kesi zinazohusu ‘kinga za haki za lazima, wajibu
na uhuru wa mtu binafsi’, uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu ya
Zanzibar “... utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama
ya Rufaa ya Tanzania.”
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya Muungano kinataja
‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo kumi na moja ya Muungano. Na
hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya
Muungano. Ijapokuwa ‘ulinzi’ ulichakachuliwa baadae kwa kuongezwa maneno
‘na usalama’, bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi na polisi
ni masuala halali ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali ya
Muungano.
Na kwa sababu hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya
Muungano kutamka – kama inavyofanya katika ibara ya 33(2) - kwamba ‘Rais
(wa Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na
Amiri Jeshi Mkuu.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, katika
kile kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya
Muungano na Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya
Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.’
Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya 121(2) ni Jeshi la Kujenga
Uchumi (JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Chuo cha Mafunzo
(cha wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo Rais wa Zanzibar
anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa....’ Kuthibitisha kwamba Idara
Maalum ni majeshi, ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum
‘... kujishughulisha na mambo ya siasa....’ Makatazo haya hayatofautiani
na makatazo ya wanajeshi kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika
ibara ya 147(3) ya Katiba ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar inaanzisha majeshi bali
pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hayo.
Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa Kamanda Mkuu
wa Idara Maalum na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile
anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa.” Aidha, kwa
mujibu wa ibara ya 123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara
ndogo ya (1) yanaingiza “... uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli
yoyote inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya Taifa.”
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haya ni mamlaka ya
kutangaza au kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya
Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele
ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hii ya ibara ya 123 ya Katiba mpya ya
Zanzibar ni sahihi.
Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali itoe tamko Bungeni ni kwa nini imeiruhusu
Zanzibar kujinyakulia mamlaka juu ya mambo ya ulinzi na usalama ambayo
kwa historia yote ya Muungano yamekuwa ni mamlaka pekee ya Serikali ya
Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu
cha 5(1)(b) cha Sheria ya Muungano kilitamka kwamba muundo wa Serikali
ya Zanzibar utakuwa kama utakavyoamuliwa na sheria za Zanzibar pekee. Na
hivyo ndivyo ilivyokubaliwa katika aya ya (iii)(a) ya Makubaliano ya
Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo wa Serikali ya Zanzibar kutokuwepo
katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba ya Muungano imetenga Sura ya
Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la
Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’
Kwa mujibu wa Profesa Shivji katika The Legal Foundations of the
Union, Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano “... haina ulazima wowote na ni
kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako ndani ya mamlaka
pekee ya Zanzibar.” Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar – kwa usahihi
kabisa - imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba ya
Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Katiba
mpya ya Zanzibar sio tu kwamba ‘imetangaza uhuru’ wa Zanzibar kwa kuhoji
misingi muhimu ya Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba
ya Muungano, bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya
tishio lolote la Serikali ya Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka
utaratibu wa kuwepo kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu
mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa mujibu wa ibara
ya 80A(1) ya Katiba hiyo, “... Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya
mabadiliko ya Katiba kuhusiana na sharti lolote lililomo katika kifungu
chochote kilichoainishwa katika kijifungu cha (2) cha kifungu hiki,
mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.”
Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu vyote vya Sehemu
ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au dola;
kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote
vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa
mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka
yake.
Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28
kinachohusu muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne
zinazohusu Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la
Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na
vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana
nayo.
Mheshimiwa Spika,
Kuweka
masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba
mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu.
Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka
misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi
kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari.
Kwa
maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala ya
kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo
yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na
Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa
Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya
Muungano. Huku, Mheshimiwa Spika, ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila
kutaja neno uhuru! Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani!
Mheshimiwa Spika,
Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, hatuna tena nchi
moja inayozungumzwa katika Katiba ya Muungano bali tuna nchi mbili. Kwa
mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena
Mambo ya Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila
moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi
wawili viongozi wa serikali wawili. Haya yote yanakiuka moja kwa moja
Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.
Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar,
Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande
wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua
Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama ya Rufani ya
Tanzania – licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba
ya Muungano - haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa
zinazohusu haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar.
Yote haya hayapo katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano
lakini yapo katika Katiba ya Muungano.
KURUDISHWA KWA SERIKALI YA TANGANYIKA
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni yetu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha jinsi ambavyo
“tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano imetiliwa nguvu kubwa na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ambayo imeipa Zanzibar nafasi na ushawishi mkubwa katika utungaji
wa Katiba Mpya.”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilionyesha kwamba, kwa mujibu wa Sheria hiyo, “Rais wa Zanzibar sio tu
kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia
ana kura ya turufu katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.” Aidha,
tulithibitisha jinsi ambavyo “... ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii
katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake (bali)
Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo
nayo katika vyombo vingine vinavyoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba....”
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia tena tahadhari iliyoitoa wakati huo
kwamba: “Masharti haya ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana athari
kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu yanakiuka
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya
Muungano na hata Katiba ya sasa ya Zanzibar....” Na kama tulivyosema
wakati huo, “... tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inarudisha mezani mjadala juu ya muundo wa
Muungano wetu na nafasi ya iliyokuwa Tanganyika katika Muungano huo.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika mazingira ambayo
upande mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru kama ambavyo tumeonyesha
hapa, huu ni wakati muafaka kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika.
Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano sio tu una
Serikali kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera
ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari
linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda
mzuri kwa Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya. Katika mazingira kama
haya, Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na
vitu vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika
hali ya usawa.
Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa
Serikali ya Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama
Kimoja au Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama
ilivyopendekezwa na Kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa
mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo
kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!
KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba inaielekeza Tume ya Katiba kuongozwa na misingi
mikuu ya kitaifa ya kuhifadhi na kudumisha ‘kuwepo kwa Jamhuri ya
Muungano.’ Hata hivyo, baada ya kujitokeza kwa wananchi wanaopinga
kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba amesema kwamba wale
wanaopinga Muungano nao wajitokeze kutoa maoni yao kwa Tume.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli mbele
ya Bunge hili tukufu ni namna gani maoni ya wale wanaotaka kiini macho
hiki cha Muungano kiishe yatashughulikiwa na Tume ambayo imepewa jukumu
kisheria la kukihifadhi na kukidumisha kiini macho hicho? Ni kipi
kitakachoizuia Tume ya Warioba kupuuza maoni ya watu hao kwa hoja kwamba
Sheria inaielekeza Tume kuratibu na kukusanya maoni na kutoa
mapendekezo ya kuhifadhi na kudumisha Muungano?
Mheshimiwa Spika,
Katika miezi ya karibuni kumejitokeza makundi ya wananchi, hasa
kwa upande wa Zanzibar, ambayo yamedai kwamba iitishwe kura ya maoni ya
wananchi ili kuamua kama bado kuna haja ya kuendelea na Muungano.
Makundi haya, yakiongozwa na kundi la Uamsho, yameshambuliwa sana
hadharani kwa kudaiwa kwamba yanataka kuvunja Muungano. Na watu ambao
wameongoza mashambulizi dhidi ya wana-Uamsho ni viongozi waandamizi wa
CCM, wakiwemo viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho.
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada
wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulisema kwamba “... hofu ... ya
kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na
ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano - juu ya ukiukwaji mkubwa wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi
ya Katiba ya Zanzibar, 2010.” Naomba nikiri kwamba tulikosea kusema
hivyo.
Tulichotakiwa kusema wakati ule, na
tunachokisema sasa, ni kwamba kimya kikuu ndani ya CCM na ndani ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya ukiukwaji mkubwa wa Makubaliano
ya Muungano na Sheria ya Muungano pamoja na Katiba kinatokana sio tu na
‘hofu’ ya kuwaudhi Wazanzibari bali pia kinatokana na ukweli kwamba
viongozi waandamizi wa CCM pamoja na wa Serikali yake walishiriki katika
ukiukwaji huo!
Wao ndio wanaoongoza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na ndio waliondaa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko
ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar. Na wao ndio wanaoongoza Serikali ya
Jamhuri ya Muungano waliokula kiapo cha kuihifadhi, kuilinda na kuitetea
Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kwa hiyo wao ndio walioiruhusu
Zanzibar kutangaza uhuru kwa Mabadiliko haya ya Katiba yake.
Mheshimiwa Spika,
Kwa viongozi hawa na chama chao kuibuka sasa na kuwatuhumu
wana-Uamsho na makundi mengine kwamba wanataka kuvunja Muungano kwa
kudai kura ya maoni ya wananchi wakati wao wenyewe wamekaa na kupitisha
marekebisho ya Katiba ambayo tayari yamevunja Makubaliano ya Muungano,
Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano ni kilele cha juu cha unafiki
wa kisiasa. Mashabiki hawa wa Muungano waeleze walikuwa wapi wakati
Zanzibar inatangaza uhuru wake kwa kuchanachana Makubaliano ya Muungano,
Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa wale wanaodai kwamba wana-Uamsho wanataka kuvunja Muungano
kwa sababu tu ya kudai kura ya maoni, tunaomba tuwakumbushe yafuatayo.
Kwanza, kwa mujibu wa Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na
Hatima ya Tanzania: “Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani
wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu
Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa.”
Hapa
Mwalimu alikuwa anamzungumzia aliyekuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Aboud
Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy waliong’olewa madarakani mwaka 1984
baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa.’
Aidha, Mheshimiwa Spika, katika kitabu hicho hicho Mwalimu Nyerere
anasema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge hili hili wakati wa
Bunge la bajeti la mwaka 1993: “Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano
wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa
taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai (kwamba)
kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa
upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano....
Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge ... liazimie kwamba
Serikali ... ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha
katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya
Tanganyika’ ndani ya Muungano.... Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge
wahusika waliwasilisha taarifa nyingine ... iliyokuwa inalitaka Bunge
... liazimie kwamba Serikali ... iandae kura ya maoni ambayo itafanyika
kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu
ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano....”
Pili, Mheshimiwa Spika, Katiba ya sasa ya Zanzibar ambayo
mashabiki wa Muungano wameileta kwa kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Kumi
ya Katiba tayari imewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kuamua, kwa kura
ya maoni, mambo mbali mbali yanayoihusu nchi hiyo na namna
itakavyoongozwa. Mashabiki hawa wa Muungano wakubali kuvuna
walichopanda, wasibeze wale wote wanaotaka kutumia haki ya kura ya maoni
kuamua hatma ya Muungano na nafasi ya Zanzibar ndani au nje yake.
Mheshimiwa Spika,
Ni wazi, kwa kuzingatia ushahidi huu, kwamba madai ya kuwa na
kura ya maoni ya wananchi ili kuamua masuala makubwa yanayohusu Muungano
wetu ni ya siku nyingi na yametolewa na watu na taasisi mbali mbali.
Madai haya hayajaanzishwa na wana-Uamsho wala CHADEMA. Ni wazi vile vile
kwamba kura ya maoni inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya
Zanzibar.
Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaungana na wale wote ambao wamedai, na wanaendelea kudai
kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakbala wa nchi
yetu. Kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati Serikali zote mbili
na chama tawala cha CCM wanauvunja kivitendo kutaipelekea nchi yetu
kwenye njia ya Ethiopia na Eritrea, au Sudan na Sudan Kusini au
Yugoslavia ya zamani.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado wanataka
kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni ndio, ni muundo gani wa
Muungano wanautaka. Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne ya
Muungano inatosha basi itakuwa afadhali kwenda njia ya Czechoslovakia ya
zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au Ethiopia na
Eritrea au Sudan na Sudan Kusini.
Mwisho, Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze
Watanzania juu ya hatua, kama zipo, ilizozichukua kuzuia ukiukwaji huu
wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba. Na mwisho,
Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama - kwa ukiukwaji huu
wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano –
Bunge hili tukufu litakuwa ndani ya mamlaka yake kuchukua hatua za
kumshtaki Rais kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba kwa kushindwa
kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Muungano kama kiapo cha kazi
yake kinavyomtaka.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano
uliowezesha maandalizi ya maoni haya. Aidha, niwashukuru familia yangu –
mke wangu mpenzi Alicia Bosensera na mapacha wetu Agostino Lissu na
Edward Bulali – kwa kuendelea kuvumilia upweke unaotokana na ‘Daddy’
kuwa mbali muda mwingi kwa sababu ya majukumu mazito ya kibunge.
Aidha, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida
Mashariki kwa imani na nguvu wanayonipa kila siku kwa kuendeleza msimamo
wetu thabiti wa kukataa kunyanyaswa, kunyonywa na kupuuzwa na ‘Ndaa ya
Njou’! Mwisho naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama
na wapenzi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote
wa Tanzania ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika
kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu. Ninawaomba waendelee
kutuunga mkono na kututia nguvu katika siku ngumu na za majaribu makubwa
zinazokuja!
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
No comments:
Post a Comment